News-Details

News >Details

CHUO KIKUU MZUMBE NA CHUO KIKUU CHA MISSISSIPPI VALLEY MAREKANI WASAINI MAKUBALIANO YA USHIRIKIANO

CHUO KIKUU MZUMBE NA CHUO KIKUU CHA MISSISSIPPI VALLEY MAREKANI WASAINI MAKUBALIANO YA USHIRIKIANO

Chuo Kikuu Mzumbe kimeingia katika hatua mpya ya kuimarisha hadhi yake kimataifa baada ya kusaini rasmi makubaliano ya Ushirikiano na Chuo Kikuu cha Mississippi Valley cha Marekani, kwenye hafla iliyofanyika leo tarehe 29 Septemba 2025 katika Ndaki ya Mbeya, na kushuhudiwa na viongozi wa vyuo hivyo, wanataaluma, pamoja na wageni waalikwa. Tukio hilo limeweka msingi wa ushirikiano wa kitaaluma utakaogusa nyanja mbalimbali ikiwemo ubadilishanaji wa walimu na wanafunzi, tafiti za pamoja, uandishi wa machapisho ya kitaaluma, pamoja na kuendeleza mitaala mipya inayojibu mahitaji ya dunia ya sasa. Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha, alisema makubaliano hayo ni hatua muhimu ya kimkakati katika kujenga nafasi ya chuo kikuu Mzumbe katika ramani ya elimu ya juu duniani. “Ushirikiano huu utatufanya tusimame kifua mbele tukiwa ni miongoni mwa vyuo vikuu vya Afrika vinavyoshirikiana kimataifa. Hii ni njia ya kuhakikisha tunazalisha wasomi wenye uwezo wa kushindana duniani kote,” alisema Prof. Mwegoha. Kwa upande wake, Rasi wa Ndaki ya Mbeya, Prof. Henry Mollel, alisisitiza kuwa makubaliano hayo ni ushindi mkubwa kwa vijana wa Ndaki hiyo, kwani yatafungua mlango wa mitaala mipya, mbinu za ufundishaji za kisasa na ushiriki wa moja kwa moja kwenye tafiti za ubunifu. “Hii ni fursa ya kipekee kwa wanafunzi wetu wa Mbeya kupata uzoefu wa kimataifa bila kulazimika kutoka nje mara kwa mara. Tunajivunia kuwa kitovu cha ushirikiano huu,” alisema Prof. Mollel. Naye, Mkuu wa Idara ya Masomo ya Biashara, Dr. Sarikiael Nnko, alieleza kwa kina historia ya majadiliano ya ushirikiano huo, ambayo yalianza mwaka 2014 na hatimaye yamezaa matunda. “Leo tunaandika historia mpya. Safari ya takribani miaka kumi sasa imefikia hitimisho, na hatua inayofuata ni utekelezaji wa miradi ya pamoja, kuandaa machapisho ya kisayansi, na kuwapeleka wanafunzi wetu kushiriki uzoefu wa kimataifa,” alisema Dr. Nnko. Akizungumza kwa niaba ya Chuo Kikuu cha Mississippi Valley cha Marekani, Prof. Kathie Stromile Golden, Makamu wa Rais Mwandamizi wa Masuala ya Taaluma, alisema chuo chake kimejipatia heshima kubwa ya kushirikiana na Mzumbe licha ya changamoto za rasilimali. Aliongeza kuwa makubaliano hayo yataweka msingi wa miradi mipya katika maeneo ya teknolojia ya akili bandia, afya ya mazingira, pamoja na masuala mapana ya kijamii. “Tunataka kuona ushirikiano huu ukibadilika kuwa mradi halisi wenye matokeo kwa jamii za Afrika na Marekani kwa pamoja,” alisema Prof. Golden. Makubaliano haya yanatarajiwa kudumu kwa miaka mitano ya awali na yataweka msingi wa kuimarisha hadhi ya kimataifa ya Chuo Kikuu Mzumbe, sambamba na kusaidia Chuo Kikuu cha Mississippi Valley cha Marekani kupanua wigo wake barani Afrika.

None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None