News-Details

News >Details

BARAZA LA CHUO KIKUU MZUMBE LAKAGUA MIRADI YA MAENDELEO KAMPASI KUU

BARAZA LA CHUO KIKUU MZUMBE LAKAGUA MIRADI YA MAENDELEO KAMPASI KUU

Baraza la Chuo Kikuu Mzumbe likiongozwa na Mwenyekiti wake, Prof. Saida Yahya-Othman, leo tarehe 2 Oktoba 2025 limefanya ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika Kampasi Kuu ya Chuo, mkoani Morogoro. Ziara hiyo pia imehudhuriwa na Wajumbe wa Menejimenti ya Chuo pamoja na wakandarasi na wasimamizi wa miradi hiyo. Katika ziara hiyo, wajumbe wamepata fursa ya kujionea hatua za utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati inayolenga kuboresha mazingira ya ujifunzaji, kufundishia na ustawi wa jamii ya Chuo. Miradi iliyotembelewa ni pamoja na ukarabati wa Hosteli ya Nyirenda, ukarabati wa viwanja vya michezo, na ukarabati wa jengo la Lumumba. Aidha, wajumbe walitembelea Kituo cha Ubora katika Ufundishaji na Ujifunzaji, ujenzi wa jengo la upasuaji katika Kituo cha Afya Mzumbe, ukarabati wa barabara za ndani za Chuo, pamoja na ujenzi wa miundombinu ya majitaka. Miradi mingine ni ujenzi wa tenki la kuhifadhi maji lenye ujazo wa lita milioni 1.6, ujenzi wa jengo la taaluma na ujenzi wa jengo la TEHAMA. Wajumbe wameonyesha kuridhishwa na kasi ya utekelezaji na ubora wa miradi hiyo, wakisisitiza kuwa itakuwa chachu ya kuinua zaidi hadhi ya Chuo Kikuu Mzumbe kitaifa na kimataifa. Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. William Mwegoha, alisema miradi hiyo ni sehemu ya mkakati wa Chuo kuhakikisha kinaendelea kuwa kitovu cha elimu bora, utafiti na huduma za kitaalamu. “Tunataka kuona kila mradi unaoanzishwa unakamilika kwa viwango vya juu na unaleta tija kwa wanafunzi, wafanyakazi na jamii kwa ujumla,” alisema Prof. Mwegoha. Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza, Prof. Saida Yahya-Othman, alipongeza jitihada zinazofanywa na Menejimenti ya Chuo katika kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati. Alibainisha kuwa uwekezaji huo mkubwa katika miundombinu ya kitaaluma na kijamii utaimarisha mazingira ya kazi na kujifunzia, jambo litakaloongeza mvuto wa Chuo kwa wadau wake. Ameitaka Menejimenti kuhakikisha kuwa miradi ya ujenzi inazingatia miundombinu rafiki kwa mazingira ikiwa ni pamoja na matumizi ya nishati ya jua. Hatua hii ni uthibitisho wa azma ya Chuo Kikuu Mzumbe kuchangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya elimu ya juu nchini, kupitia uwekezaji katika miundombinu na huduma bora kwa wanafunzi na jamii.

None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None