News-Details

News >Details

MRADI WA TANZIE KUCHOCHEA NA KUIMARISHA UKIMATAIFAJI ELIMU YA JUU

MRADI WA TANZIE KUCHOCHEA NA KUIMARISHA UKIMATAIFAJI ELIMU YA JUU

Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania Prof. Charles Kihampa amesema Serikali inaendelea kuimarisha mifumo ya elimu ya juu nchini ikiwa ni pamoja na kusukuma mbele agenda ya ukimataifaji. Prof. Kihampa ameyasema haya wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya siku tatu ya Mradi wa TANZIE kwa wakufunzi na kikao cha uratibu kilichofanyika Oktoba 7, 2025, katika Chuo Kikuu Mzumbe, Morogoro. Mafunzo hayo yamewakutanisha pamoja washirika kutoka Bara la Ulaya na taasisi za elimu ya juu nchini zikiwemo Chuo Kikuu Mzumbe, Chuo Kikuu Katoliki cha Afya na Sayansi Shirikishi, Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro, Taasisi ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania kwa ajili ya kujadili njia za kuimarisha ukimataifaji katika elimu. Prof. Kihampa amebainisha kuwa kwa sasa nchi ina wafanyakazi wa kitaaluma wa kimataifa 293 wanaofundisha katika vyuo vikuu mbalimbali na zaidi ya wanafunzi wa kimataifa 1,000 wanaosoma nchini. Alisisitiza kuwa Serikali imeandaa Mwongozo wa Udahili wa Wanafunzi wa Shahada ya Uzamili na Shahada za Awali, sambamba na mfumo wa kutathmini ulinganifu na utambuzi wa tuzo za wahitimu kutoka vyuo vikuu vya nje ya Tanzania, hatua zinazolenga kudumisha ubora na ushindani wa elimu ya juu nchini. Awali, Makamu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha, amesema Chuo kinajivunia kuwa mwenyeji wa mafunzo hayo muhimu, akisisitiza kuwa TANZIE ni chachu ya mageuzi katika elimu ya juu nchini. “Kupitia ushirikiano huu wa kimataifa, tunajenga taasisi zenye maono mapana, zinazochochea ubunifu, ubora na ujumuishi katika elimu ya juu,” amesisitiza Prof. Mwegoha. Mkurugenzi wa Ukimataifaji na Baraza la Wahitimu Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Lucy Massoi, amesema mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi, ambapo unalenga kujenga uwezo wa ndani kupitia wakufunzi wa kitaifa watakaosambaza mbinu bora za kimataifa. “Kupitia TANZIE, tunatengeneza kizazi kipya cha wabobezi wa elimu watakaowezesha vyuo vikuu vya ndani kujiendesha kwa ubora wa kimataifa,” alisema Dkt. Massoi. Uzinduzi wa Mafunzo ya kwanza kwa Wakufunzi chini ya Mradi wa TANZIE unaashiria hatua kubwa kuelekea kuimarisha elimu ya juu inayounganisha Tanzania na dunia katika ushirikiano wa kitaaluma, utafiti na maendeleo endelevu.

None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None