News-Details

News >Details

MZUMBE YAKUSANYA MAONI YA UWEKEZAJI WA PPP MKINGA, YAPONGEZWA NA MKUU WA MKOA WA TANGA

MZUMBE YAKUSANYA MAONI YA UWEKEZAJI WA PPP MKINGA, YAPONGEZWA NA MKUU WA MKOA WA TANGA

Timu ya Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) kutoka Chuo Kikuu Mzumbe imefanya ziara mkoani Tanga, Oktoba 09, 2025, kwa ajili ya kukusanya maoni ya wadau kuhusu namna bora ya kutekeleza uwekezaji wa ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP) katika kuendeleza Kampasi mpya ya Mzumbe mkoani Tanga. Ziara hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mikakati ya chuo katika kuimarisha miundombinu na kuboresha mazingira ya utoaji elimu ya juu nchini. Timu hiyo imeongozwa na Mratibu wa Mradi wa HEET Chuo Kikuu Mzumbe Prof. Hawa Tundui na kuambatana na Naibu Mratibu wa Mradi wa HEET Chuo Kikuu Mzumbe Dkt. Lihoya Chamwali, Mratibu wa Mradi wa HEET upande wa Ujenzi Msanifu majengo Bw. Joseph Ng’wala na Mratibu wa Mradi wa HEET upande wa mahusiano ya kazi na sekta binafsi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Timu ya Kukusanya Maoni ya PPP) Dkt. Albogast Musabila. Aidha, timu hiyo ilipata fursa ya kukutana na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian, ambaye alipongeza juhudi za Chuo Kikuu Mzumbe katika kuendeleza miradi ya kimkakati ya elimu ya juu inayolenga kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi mkoani humo. Mhe. Dkt. Burian alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga, Jiji la Tanga na Chuo Kikuu Mzumbe katika kuweka mipango thabiti ya kuhakikisha miundombinu na huduma muhimu zinapatikana kabla ya kuanza kwa masomo. Kwa upande wake, Dkt. Musabila alieleza kuwa timu hiyo inakusanya maoni kutoka kwa wadau mbalimbali ili kubaini fursa na changamoto za utekelezaji wa miradi kwa mfumo wa PPP, hasa katika kuhakikisha mazingira ya uwekezaji yanakuwa rafiki kwa sekta binafsi kushiriki katika maendeleo ya elimu. Kupitia ziara hiyo, Mzumbe inaona umuhimu mkubwa wa kushirikiana na wadau wa maendeleo, hususan Serikali za Mitaa na sekta binafsi, katika kuhakikisha mradi wa Kampasi ya Tanga unakuwa wa mfano wa mafanikio ya ushirikiano wa ubia nchini. Ushirikiano huo unatarajiwa kuleta matokeo chanya katika elimu, uchumi na maisha ya wananchi wa Mkoa wa Tanga.

None
None
None
None