Chuo Kikuu Mzumbe, kupitia Taasisi ya Taaluma na Maendeleo (Institute of Development Studies - IDS), kimeendelea kuthibitisha hadhi yake kama kitovu cha tafiti bunifu na zenye tija kwa jamii baada ya Bi. Rofina Mrosso kufanikiwa kutetea kwa mafanikio makubwa tasnifu yake ya Shahada ya Uzamivu (PhD) tarehe 7 Oktoba 2025. Tasnifu yake, iliyokuwa na mada “Ubunifu na Utendaji wa Biashara Zinazoongozwa na Wanawake katika Sekta Ndogo ya Uchakataji Chakula Nchini Tanzania: Nafasi ya Kati ya Uwezo wa Mabadiliko”, imechambua kwa kina mchango wa ubunifu na uwezo wa mabadiliko (transformative capacity) katika mafanikio ya biashara zinazoendeshwa na wanawake wajasiriamali nchini. Katika utafiti wake, Bi. Mrosso ameeleza kuwa wanawake wengi katika sekta ya uchakataji wa chakula nchini Tanzania wana mawazo ya kibunifu, lakini “changamoto kubwa ipo katika kuyageuza mawazo hayo kuwa mikakati inayotekelezeka, yenye matokeo endelevu.” Amebainisha kuwa uwezo wa mabadiliko ni kipengele muhimu kinachowawezesha wanawake kuhimili ushindani, kubadilika kulingana na mazingira ya soko, na kutumia ubunifu kama chachu ya maendeleo ya biashara zao. “Ubunifu pekee haukamilishi safari ya mafanikio ya kiuchumi — ni uwezo wa kubadilika na kukabiliana na vikwazo vinavyoamua kama biashara itastawi au itadumaa,” alisema Bi. Mrosso wakati wa utetezi wake. Ameongeza kuwa, kwa wanawake wengi, maendeleo ya biashara zao yamekuwa yakikwamishwa na changamoto za mitaji, teknolojia duni, na ukosefu wa mafunzo ya kisasa ya biashara. “Tunapaswa kuwekeza katika kuimarisha uwezo wa wanawake kubadilika, kujifunza na kuboresha bidhaa zao kwa kuzingatia ubora, thamani, na mahitaji ya soko.” Utafiti huo pia umependekeza kuwa taasisi za kifedha na za maendeleo zitoe mikopo rafiki, huduma za ushauri, na programu za kujenga uwezo zitakazowawezesha wanawake kuendesha biashara zenye tija na ubunifu endelevu. Baada ya utetezi wa kina uliohudhuriwa na wataalamu na wanataaluma mbalimbali, Bi. Mrosso alitangazwa rasmi kuwa amefaulu kwa mafanikio makubwa kutetea tasnifu yake ya PhD, chini ya Mwenyekiti wa jopo lililoongozwa na Profesa Theobald Frank Theodory. Msimamizi mkuu wa utafiti huo alikuwa Profesa Elizabeth Lulu Genda, huku Dkt. Nicholaus Tutuba akiwa msimamizi msaidizi. Wanajopo wengine walikuwa: Mtahini wa Nje, Prof. Justine Urassa; Mtahini wa Ndani, Dkt. Athanas Ngalawa; Kaimu Mkurugenzi wa Idara za Maendeleo, Dkt. Noebert Ngowi; na Mkuu wa Idara ya Sera za Maendeleo, Dkt. Moses Ndunguru. Kwa upande wake, Dkt. Ngowi alisisitiza kuwa utafiti huo unatoa mchango wa kipekee katika sera na mipango ya maendeleo ya wanawake nchini Tanzania. “Tasnifu hii siyo tu kazi ya kitaaluma, bali ni dira ya kubadilisha fikra kuhusu nafasi ya wanawake katika sekta ya viwanda vidogo na uchakataji wa chakula,” alifafanua. Hatua hii ya mafanikio ya Bi. Rofina Mrosso inaendelea kuthibitisha dhamira ya Chuo Kikuu Mzumbe katika kuandaa watafiti wabunifu na wenye mchango wa moja kwa moja katika ustawi wa jamii kwakuwa chimbuko la maarifa na ubunifu unaolenga kubadilisha maisha ya Watanzania. Chuo Kikuu Mzumbe, Tujifunze kwa Maendeleo ya Watu.