Chuo Kikuu Mzumbe kimezindua rasmi kampeni ya chanjo ya homa ya ini kwa kuwachanja Watumishi wake ikiwa ni utekelezaji wa mpango mkakati wake wa maendeleo unaoelekeza kuweka mazingira salama kwa Watumishi kwa kuwakinga na magonjwa mbalimbali yakiwemo ya kuambukiza na yasiyoambukiza Akizindua Kampeni hiyo tarehe 6 Oktoba, 2025 Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. William Mwegoha alisema dhamira ya Chuo ni kuhakikisha watumishi wote wanakuwa salama nyakati zote ili kuwawezesha kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kufafanua kuwa hiyo ndiyo sababu iliyopelekea Chuo kugharamia chanjo za homa ya ini kwa Watumishi wake wote na aliwahimiza Watumishi kutumia fursa hiyo kwa kupata kinga dhidi ya ugonjwa wa homa ya ini ambao unaelezwa kuwa kwa sasa umekuwa tishio Kwa upande wake, Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma, Utafiti na Ushauri, Prof. Idda Lyatonga Swai aliipongeza hatua hiyo ya utoaji chanjo, akisisitiza kuwa elimu ya afya ni msingi wa kuzuia magonjwa kazini. Alihimiza watumishi kuitumia fursa hii kama sehemu ya kujilinda na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao. Naye Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo - Mipango Fedha na Utawala Dkt. Joseph Sungau aliongeza kuwa kampeni hii imewezeshwa kupitia bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026, kwa lengo la kuhakikisha kila mtumishi anapata chanjo hii bure akisisitiza kuwa afya bora kwa watumishi ni msingi wa mafanikio ya taasisi. Dkt. Nyangara Rajabu Mtilly, Mkurugenzi wa Afya wa Chuo, alieleza kuwa chanjo hiyo inalenga kuzuia homa ya ini aina ya Hepatitis B, inayoenezwa kupitia damu, majimaji ya mwili na kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto. Alibainisha kuwa zoezi la chanjo litafuata utaratibu wa upimaji kabla ya mtu kupewa chanjo, ambayo hutolewa kwa awamu tatu kwa watu wazima. Zoezi hilo linaendelea katika Kampasi Kuu hadi tarehe 10 Oktoba 2025, na litaendelea katika Ndaki ya Mbeya kuanzia 13–17 Oktoba, na Ndaki ya Dar es Salaam kuanzia 20–24 Oktoba 2025.