Chuo Kikuu Mzumbe kimeungana na Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro katika Maadhimisho ya Wiki ya Sheria 2025 kwa kushiriki kikamilifu kutoa elimu na ushauri kwa wananchi katika masuala mbalimbali ya kisheria. Uzinduzi wa maadhimisho haya umefanyika tarehe 25 Januari 2025 kwa matembezi ya aina yake yaliyoanzia Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro na kumalizikia katika eneo la stendi ya zamani ya daladala, Morogoro Mjini. Katika maadhimisho hayo, Chuo Kikuu Mzumbe kupitia kituo chake cha msaada wa Sheria kilicho chini ya kitivo cha Sheria cha chuo hicho,kimepeleka wataalamu wake wa masuala ya sheria kwa ajili ya kutoa elimu na ushauri kwa wananchi kuhusu masuala muhimu yanayohusu maisha ya kila siku, ikiwemo Mirathi, Wosia, Migogoro ya Ardhi, Haki Jinai, Ukatili wa Kijinsia, Mikataba, Usuluhishi na Uwakilishi Mahakamani. Akizungumza wakati wa uzinduzi wa maadhimisho hayo, Mgeni Rasmi ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Mussa Kilakala aliipongeza Mahakama ya Tanzania na wadau wake kwa juhudi za kuimarisha mfumo wa utoaji haki kwa wananchi. Alisisitiza kuwa kaulimbiu ya mwaka huu, "Tanzania ya 2050: Nafasi ya Taasisi zinazosimamia Haki Madai katika kufikia Malengo Makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo", inahimiza dhamira ya pamoja ya kufanikisha ustawi wa taifa kwa kupitia mifumo thabiti ya haki. “Nawapongeza wadau mbalimbali kwa kushiriki kikamilifu kutoa elimu ya sheria kwa wananchi wetu. Ushiriki wenu unaonesha dhamira ya dhati ya kushirikiana na wadau wa haki katika kuhakikisha jamii inapata maarifa sahihi itakayosaidia kujenga taifa lenye haki na usawa,” alisema Mhe. Kilakala. Pia, Chuo Kikuu Mzumbe kimetumia fursa hii kueleza namna ambavyo kinatoa usaidizi wa kisheria kwa jamii kupitia kituo chake cha msaada wa sheria (legal aid clinic) kinacholenga kusaidia wananchi wa kipato cha chini. Maadhimisho ya Wiki ya Sheria mwaka huu yameanza tarehe 25 Januari na yanatarajiwa kuhitimishwa tarehe 01 Februari, huku kilele chake kikitarajiwa kufanyika tarehe 03 Februari, 2025