News-Details

News >Details

MZUMBE YAENDESHA MAFUNZO KUHUSU NISHATI JADIDIFU NCHINI TANZANIA KUPITIA MRADI WA NISHATI

MZUMBE YAENDESHA MAFUNZO KUHUSU NISHATI JADIDIFU NCHINI TANZANIA KUPITIA MRADI WA NISHATI

Chuo Kikuu Mzumbe kupitia Mradi wa Nishati kimeendesha mafunzo ya siku moja yaliyofanyika tarehe 13 Oktoba 2025 katika Kampasi Kuu ya Morogoro. Mafunzo hayo yaliendeshwa na wawezeshaji kutoka Kampuni ya Studio Santi Limited na yalihusisha baadhi ya wanataaluma, wawezeshaji, pamoja na wanafunzi wa shahada mbalimbali wa Chuo Kikuu Mzumbe. Akifungua rasmi mafunzo hayo, Kaimu Amidi wa Skuli ya Utawala wa Umma na Menejimenti wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. Mackfallen Anasel, alisisitiza umuhimu wa kuwekeza katika utafiti na matumizi ya nishati jadidifu kama nguzo muhimu ya maendeleo endelevu nchini. “Nishati jadidifu si tu mbadala wa nishati ya kisukuku, bali ni fursa ya mageuzi katika sekta ya kilimo na uchumi wa kijani. Kama taifa, tunapaswa kuendelea kuhamasisha matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira ambazo zitawawezesha wakulima na wananchi vijijini kufikia maendeleo ya kweli, ” alisema Prof. Anasel. Aidha, aliongeza kuwa Chuo Kikuu Mzumbe kimeendelea kujikita katika utafiti, ubunifu na mafunzo yanayolenga kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi, ikiwemo nishati safi, kama sehemu ya utekelezaji wa dira yake ya kutoa elimu bora na yenye matokeo chanya kwa jamii. Akiwasilisha mada ya “Ubunifu na Utekelezaji wa Mifumo ya Nishati ya Jua (Solar PV) Pamoja na Tathmini ya Athari za Mazingira na Uchambuzi wa Kiuchumi,” Mhandisi Minaclara Lwiwa kutoka Studio Santi Limited alieleza kuwa nishati ya jua ni suluhisho endelevu kwa changamoto za upatikanaji wa umeme, hasa vijijini. Alibainisha kuwa matumizi ya mifumo ya Solar PV yanaweza kupunguza gharama za uzalishaji, kulinda mazingira, na kuongeza fursa za ajira katika jamii. Kwa upande wake, Mhandisi Beatrice Mwella kutoka kampuni hiyohiyo, akiwasilisha mada ya “Rasilimali za Nishati Jadidifu Tanzania na Thamani Inayoongezwa katika Kilimo,” alifafanua namna nishati jadidifu inavyoweza kuchangia katika uongezaji thamani wa mazao ya kilimo kupitia umwagiliaji wa kisasa, usindikaji, na uhifadhi wa mazao. Alisema kuwa nishati safi ni kichocheo muhimu cha kilimo chenye tija na uendelevu wa kiuchumi kwa wakulima wadogo.

None
None
None
None
None
None
None
None
None