News-Details

News >Details

KAMPENI YA CHANJO YA HOMA YA INI YAENDELEA NDAKI YA MBEYA

KAMPENI YA CHANJO YA HOMA YA INI YAENDELEA  NDAKI YA MBEYA

Tarehe 13 Oktoba 2025, Watumishi wa Ndaki ya Mbeya wamenufaika na muendelezo wa kampeni maalum ya utoaji wa elimu na chanjo dhidi ya homa ya ini (Hepatitis B), iliyofanyika chuoni hapo. Kampeni hii ni sehemu ya mwendelezo wa uzinduzi rasmi uliofanyika tarehe 6 Oktoba 2025, ambapo Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha alizindua rasmi kampeni ya chanjo kwa watumishi wote wa Chuo kwa lengo la kuboresha afya na ustawi wa wafanyakazi. Akifungua rasmi Kampeni hiyo, Naibu Rasi wa Ndaki hiyo, Prof. Charles Tundui, ambaye aliwahimiza watumishi kuchukua tahadhari dhidi ya homa ya ini. Alisisitiza kuwa afya bora ya mtumishi ni msingi wa ufanisi katika utoaji wa huduma za elimu ya juu. “Ni jukumu letu kuhakikisha tunaweka afya mbele, na kampeni hii ni sehemu ya kuonesha kuwa Chuo kinajali usalama wa watumishi wake,” alisema Prof. Tundui. Aidha, Mkurugenzi wa Afya na Huduma za Kitabibu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Rajab Nyangara, alieleza kuwa chanjo hiyo imefadhiliwa na Taasisi kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kama sehemu ya mkakati endelevu wa kulinda afya za watumishi wake na kukuza ustawi wa taasisi kwa ujumla. Dkt. Mohamed Ayub kutoka Kituo cha Afya cha Chuo Kikuu Mzumbe alitoa elimu ya kina kuhusu namna ugonjwa wa homa ya ini unavyoambukizwa, madhara yake kwa mwili wa binadamu, pamoja na njia salama za kujikinga, ikiwemo chanjo. Akitoa neno la shukrani, Afisa Mkuu wa Rasilimali Watu wa Ndaki ya Mbeya, Bw. Lusajo Ngabo, alieleza kufurahishwa kwake na hatua hiyo muhimu kwa ustawi wa afya za watumishi. Alitoa wito kwa watumishi wote wa Ndaki hiyo kujitokeza kwa wingi kupata chanjo hiyo inayotolewa katika Zahanati ya Ndaki kuanzia tarehe 13 Oktoba 2025 hadi 17 Oktoba 2025. Watumishi wengi walijitokeza kupatiwa chanjo, hali iliyodhihirisha mwitikio chanya na uelewa kuhusu umuhimu wa kinga hiyo. Baadhi yao walipongeza hatua hiyo wakisema imewaongezea maarifa na kuwasaidia kuchukua tahadhari mapema dhidi ya ugonjwa huo hatari.

None
None
None
None
None
None
None
None
None
None