News-Details

News >Details

CHUO KIKUU MZUMBE NA TAASISI YA ACCA (UINGEREZA) WAENDELEA KUDUMISHA USHIRIKIANO WA KITAALUMA

CHUO KIKUU MZUMBE NA TAASISI YA ACCA (UINGEREZA) WAENDELEA KUDUMISHA USHIRIKIANO WA KITAALUMA

Chuo Kikuu Mzumbe kimeendelea kudumisha uhusiano wa kitaaluma na taasisi kutoka Uingereza ijulikanayo kama "Association of Chartered Certified Accountants (ACCA)". Katika kudhihirisha suala hilo, ACCA imekabidhi Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam jumla ya vitabu 69 vya mafunzo ya masomo ya uhasibu kama sehemu ya juhudi za kuimarisha ubora wa ufundishaji na ujifunzaji wa masomo ya uhasibu nchini Tanzania. Tukio hilo limefanyika katika hafla ndogo ya makabidhiano ya vitabu tajwa iliyofanyika mwishoni mwa wiki Chuoni hapo lililodhuriwa na viongozi wa pande zote mbili za taasisi. Akipokea kwa niaba ya Chuo, Naibu Rasi wa Ndaki ya Dar es Salaam, Prof. Omary Swalehe aliishukuru taasisi ya ACCA kwa msaada huo akisema kuwa vitabu hivyo vitakuwa nyenzo muhimu katika kuongeza ufanisi wa kufundisha na kujifunza masomo ya uhasibu. “Tumepokea vitabu hivi kutoka ACCA ya Uingereza, ambavyo vitatusaidia sisi walimu katika kufundishia masomo ya uhasibu, pia vitasaidia kuongeza ubora wa elimu na kuongeza uelewa wa vitendo katika taaluma ya uhasibu na kuwasaidia wanafunzi katika kuelewa masomo.” Alisema Prof. Swalehe Kwa upande wake, Bw. Jenard Lazaro, Meneja wa ACCA nchini Tanzania alisema kuwa taasisi ya ACCA imekuwa ikishirikiana kwa karibu na Chuo Kikuu Mzumbe kwa miaka kadhaa, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kukuza uwezo wa wahadhiri na wanafunzi katika taaluma ya uhasibu kitaifa, akisisitiza kuwa makabidhiano haya ya vitabu ni mwendelezo wa ushirikiano huo, lengo likiwa kuhakikisha wanafunzi wanapata vitabu vyenye ubora wa juu vitakavyochochea mafanikio yao kitaaluma. Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi na wahadhiri kutoka Chuo Kikuu Mzumbe ambao ni Dkt. Daudi Pascal Ndaki, Mwakilishi wa Mtiva wa Skuli ya Biashara kutoka Kampasi Kuu Morogoro; Dkt. Joshua Mwakujonga, Mkuu wa Idara ya Masomo ya Biashara Ndaki ya Dar es Salaam pamoja; na Bw. Elias Ntobi, Mkuu Kitengo cha Huduma za Maktaba. Chuo Kikuu Mzumbe, Tujifunze kwa Maendeleo ya Watu

None
None
None