News-Details

News >Details

JUVENALIS MWOMBEKI AFANIKIWA KUTETEA TASNIFU YAKE YA UZAMIVU – ABUNI MFUMO WA KIDIGITALI KUFUATILIA MABADILIKO YA IDADI YA WATU NCHINI

JUVENALIS MWOMBEKI AFANIKIWA KUTETEA TASNIFU YAKE YA UZAMIVU – ABUNI MFUMO WA KIDIGITALI KUFUATILIA MABADILIKO YA IDADI YA WATU NCHINI

Bw. Juvenalis Mwombeki, mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) kutoka Kitivo cha Sayansi na Teknolojia (FST), Chuo Kikuu Mzumbe, amefanikisha kwa mafanikio makubwa utetezi wa tasnifu yake yenye kichwa “Matumizi ya Teknolojia Dijitali katika Kuwezesha Ufuatiliaji wa Mabadiliko ya Idadi ya Watu: Mfano Tanzania". Utetezi huo umefanyika tarehe 20 Oktoba 2025 katika Kampasi Kuu Morogoro, mbele ya jopo la watahini lililoongozwa na Prof. Emmanuel Ndikumana. Katika utafiti wake, Bw. Mwombeki amebuni mfano wa kiteknolojia unaolenga kuboresha mfumo wa ukusanyaji na uchambuzi wa taarifa za mabadiliko ya idadi ya watu nchini Tanzania kwa njia ya kidigitali. Utafiti huo unalenga kuongeza usahihi, ufanisi na uharakishaji wa upatikanaji wa takwimu muhimu kwa ajili ya kupanga maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Akizungumza wakati wa utetezi, Bw. Mwombeki alieleza kuwa teknolojia ya kidigitali ni chachu muhimu katika kusaidia serikali na taasisi mbalimbali kufuatilia mienendo ya idadi ya watu kwa wakati halisi, jambo litakalosaidia katika kupanga sera na mikakati ya maendeleo kwa ufanisi zaidi. Msimamizi Mkuu wa Utafiti huo alikuwa Dkt. Patrick D. Kihoza, huku Msaidizi wa Msimamizi wa Utafiti akiwa Dkt. Morice Daudi. Wote walimpongeza mwanafunzi huyo kwa ufanisi na ubunifu mkubwa aliouonyesha katika kubuni mfumo unaoweza kuchangia maboresho katika ukusanyaji wa takwimu nchini. Baada ya majadiliano ya kina, Mwenyekiti wa jopo la watahini, Prof. Emmanuel Ndikumana, alimtangaza Bw. Juvenalis Mwombeki kuwa amefaulu kwa kiwango cha kuridhisha kutetea tasnifu yake, akisisitiza kuwa matokeo ya utafiti wake ni nyenzo muhimu katika juhudi za taifa kuelekea uchumi wa kidigitali. Hatua hii inaendelea kuthibitisha dhamira ya Chuo Kikuu Mzumbe katika kukuza utafiti, ubunifu, na matumizi ya teknolojia katika kuleta suluhisho bunifu kwa changamoto za kijamii na kiuchumi nchini.

None
None
None
None
None
None