Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. Allen Mushi, amebainisha kuwa uongozi wa chuo unaendelea kuhakikisha usalama wa watu na mali mahali pa kazi kwa kuandaa mafunzo yanayowaelimisha watumishi kuhusu usalama kazini na maandalizi ya dharura katika sehemu zote za kazi. Ameyasema hayo wakati akifungua rasmi Mafunzo ya Tahadhari na Kinga ya Majanga, hususani ya moto, yaliyofanyika Oktoba 20, 2025 katika Kampasi Kuu ya Morogoro. Mafunzo hayo, yaliyoandaliwa kwa kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro, yalilenga kuwajengea watumishi ujuzi na uelewa wa kukabiliana na majanga ya moto, kulinda maisha ya watu, na kuzuia uharibifu wa mali. Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Afisa wa Kitengo cha Elimu kwa Umma wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Koplo Emmanuel Sipalika alisisitiza umuhimu wa kila taasisi kuwa na utaratibu wa usalama wa moto, kuwa na vifaa vya kuzimia moto pamoja na mpango wa dharura utakaosaidia kupunguza madhara pindi ajali inapotokea. Pia, Koplo Sipalika alikumbusha kuwa huduma zinazotolewa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ni bure, na akawahimiza wananchi kutumia namba ya dharura 114 mara wanaposhuhudia ajali au majanga ya moto, ili kurahisisha uokoaji wa maisha na mali kwa haraka. Aidha, alitoa mafunzo kwa vitendo juu ya matumizi sahihi ya bomba maalumu la maji kwa kuzimia moto (fire hose reel) katika kudhibiti moto wa awali kabla haujasambaa. Kwa upande wake, Mkaguzi Msaidizi Anclet Mzeru alitoa mafunzo ya vitendo namna ya matumizi ya Mtungi wa kuzima moto wa awali, akionyesha hatua za namna ya kukabiliana na moto wa awali kabla haujasambaa. Mafunzo hayo kwa vitendo yalisaidia washiriki kujifunza mbinu sahihi za kutumia vifaa vya kuzimia moto kwa usalama na ufanisi. Miongoni mwa mada zilizofundishwa ni pamoja na utoaji wa huduma ya kwanza kwa waathirika wa moto, ukaguzi wa usalama wa majengo, namna ya kutoa taarifa za haraka wakati wa dharura, na hatua za kuchukua katika kuhakikisha usalama wa watu na mali. Kupitia ushirikiano huu na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Chuo Kikuu Mzumbe kinaendelea kujenga mazingira salama na endelevu ya kazi.