News-Details

News >Details

KAMPENI YA CHANJO YA HOMA YA INI YAENDELEA NDAKI YA DAR ES SALAAM

KAMPENI YA CHANJO YA HOMA YA INI YAENDELEA NDAKI YA DAR ES SALAAM

Chuo Kikuu Mzumbe kimeendelea kutekeleza Kampeni ya Chanjo ya Homa ya Ini (Hepatitis B), kwa watumishi wa Ndaki ya Dar es Salaam, ikiwa ni mwendelezo wa juhudi za kutoa elimu na huduma ya chanjo dhidi ya ugonjwa huo. Zoezi hilo linaendelea tangu Oktoba 20, 2025 na kufikia tamati ifikapo Oktoba 24,2025 Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo katika Ndaki ya Dar es Salaam, Kaimu Rasi wa Ndaki hiyo, Prof. Omary Swalehe, aliwataka watumishi kuchukua hatua za kujilinda dhidi ya homa ya ini. Alisisitiza kuwa afya njema ni nyenzo muhimu katika kuongeza ufanisi wa kazi na ubora wa huduma zinazotolewa na Chuo. “Afya bora ya mtumishi ni nguzo ya mafanikio katika taasisi yoyote; ni jukumu letu kila mmoja kuhakikisha tunajilinda dhidi ya magonjwa yanayoweza kuzuilika,” alisema Prof. Swalehe. Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Afya na Huduma za Kitabibu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Rajab Nyangara, alieleza kuwa lengo kuu la kampeni hiyo ni kuongeza uelewa kuhusu ugonjwa wa homa ya ini na kuhamasisha watumishi wote kujikinga kupitia chanjo. Alibainisha kuwa ugonjwa huo ni miongoni mwa magonjwa hatari yanayoweza kudhoofisha ini na kusababisha madhara makubwa kiafya, ikiwemo kifo endapo hautatibiwa mapema. Vilevile, Dkt. Mohamed Ayub kutoka Kituo cha Afya cha Chuo Kikuu Mzumbe alitoa elimu ya kina kuhusu njia za maambukizi ya homa ya ini, athari zake katika mwili wa binadamu, pamoja na mbinu salama za kujikinga, ikiwemo upatikanaji wa chanjo kamili kwa wakati. Akizungumza wakati wa kutoa shukrani, Mkuu wa Idara ya Huduma za Kiutawala wa Ndaki ya Dar es Salaam, Bi. Janeth Mumangi, alionesha kuridhishwa na mwitikio wa watumishi katika kampeni hiyo. Alihimiza watumishi wote kuhakikisha wanapata chanjo katika kipindi kilichopangwa, ili kuepuka hatari ya kupata maambukizi ya homa ya ini. Kampeni hii ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa baada ya uzinduzi rasmi uliofanyika tarehe 6 Oktoba 2025, ambapo Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha, alizindua rasmi mpango wa chanjo kwa watumishi wote wa Chuo, kwa lengo la kuboresha afya, kuongeza tija kazini na kukuza ustawi wa watumishi.

None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None