Chuo Kikuu Mzumbe kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) wamezindua Mradi wa Kusaidia Uhifadhi wa Mfumo Ikolojia wa Tanganyika na Urejeshaji wa Malisho (STE & GRL), uliofadhiliwa na Shirika la Ushirikiano wa Maendeleo la Norway (Norad) na kuratibiwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH). Uzinduzi huo umefanyika tarehe 21 Oktoba 2025 Mkoani Katavi. Mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Mhe. Onesmo Buswelu, akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko, aliipongeza COSTECH, TALIRI na Mzumbe University kwa ubunifu na dhamira ya kulinda mfumo ikolojia wa Tanganyika. Alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali, taasisi za utafiti na wananchi katika kulinda mazingira na kuboresha maisha ya jamii. Awali Mratibu wa Mradi kutoka Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. Frank Theobard alieleza kuwa mradi unalenga kupata uelewa wa awali wa hali ya sasa kufuatia uhamaji wa wakulima na wafugaji na kuanzisha hatua za kupunguza athari hasi kwa ustawi endelevu wa maisha ya wananchi. Alibainisha kuwa utekelezaji wa mradi utahusisha uanzishwaji wa shamba darasa kwa ajili ya mafunzo ya vitendo na uhamasishaji wa mbinu bora za uhifadhi wa mazingira. Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TALIRI, Dkt. Andrew Chota, alisema taasisi hiyo imejipanga kitaalamu na kitaasisi kushirikiana na wadau kuhakikisha teknolojia bora za ufugaji na kilimo hifadhi zinawafikia walengwa kwa wakati. Naye Mwakilishi wa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Nsubili Isaga, alisema Mzumbe inathamini miradi ya kimkakati kama huu kwani inaongeza mchango wa kitaaluma, ubunifu na tafiti zenye suluhisho la changamoto za jamii. Alisisitiza utayari wa Mzumbe kutoa wataalamu na rasilimali kufanikisha utekelezaji wake. Baada ya hotuba hizo, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi, Bw. Florence Chrisant, alitoa shukrani kwa waandaaji na wadau wote walioufanikisha uzinduzi huo, akiahidi ushirikiano wa serikali ya mkoa katika utekelezaji wa mradi huo.