News-Details

News >Details

BI. HAPPINESS YORAM GEFI AIBUKA KIDEDEA KATIKA UTETEZI WA TASNIFU YAKE YA UZAMIVU

BI. HAPPINESS YORAM GEFI AIBUKA KIDEDEA KATIKA UTETEZI WA TASNIFU YAKE YA UZAMIVU

Kutetea tasnifu ya Uzamivu ni hatua muhimu katika safari ya kitaaluma inayodhihirisha ubobezi, maarifa, na mchango wa kitafiti kwa jamii. Hatua hii imefikiwa kwa mafanikio makubwa na Bi. Happiness Yoram Gefi, mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) kutoka Taasisi ya taaluma za maendeleo (IDS), Chuo Kikuu Mzumbe, ambaye amefanikiwa kutetea tasnifu yake kwa ufanisi wa hali ya juu. Utetezi huo umefanyika tarehe 28 Oktoba 2025 katika Kampasi Kuu ya Morogoro, mbele ya jopo la watahini lililoongozwa na Profesa Frank Theobald. Utafiti huo, uliokuwa chini ya usimamizi wa Daktari Moses Ndunguru (Msimamizi Mkuu) na Profesa Elizabeth Lulu Genda (Msimamizi Msaidizi), umebeba mada isemayo “Mchango wa taasisi za kidini katika kupambana na ukatili wa kingono dhidi ya wasichana balehe nchini Tanzania: Uzoefu kutoka jamii za wafugaji mkoa wa Manyara.” Kupitia utafiti wake, Bi. Happiness ameonyesha kwa kina namna taasisi za kidini zinavyoweza kuwa nguzo muhimu katika kupunguza na kutokomeza ukatili wa kingono dhidi ya wasichana balehe, hasa katika jamii za wafugaji. Amebainisha kuwa taasisi hizo zina mchango mkubwa kupitia elimu, malezi, maadili, na ushawishi wa kijamii unaoweza kubadili mitazamo potofu kuhusu jinsia na haki za mtoto wa kike. Akizungumza wakati wa utetezi wake, Bi. Happiness alisisitiza kuwa mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia yanahitaji ushirikiano wa wadau wote, wakiwemo viongozi wa dini, serikali, na jamii kwa ujumla, ili kujenga mazingira salama kwa wasichana, hasa katika maeneo yenye mila na desturi kandamizi. Baada ya mjadala wa kina, Profesa Frank Theobald, Mwenyekiti wa jopo la watahini, alimtangaza rasmi Bi. Happiness kuwa amefaulu kutetea tasnifu yake kwa kiwango cha kuridhisha, akieleza kuwa matokeo ya utafiti wake ni nyenzo muhimu katika kuimarisha sera na mikakati ya kulinda haki za watoto wa kike nchini. Mafanikio haya yanaendeleza dhamira ya Chuo Kikuu Mzumbe, kupitia Taasisi ya Taaluma za Maendeleo (IDS), katika kuzalisha watafiti wabobezi na wabunifu wanaotoa suluhisho la kisayansi kwa changamoto za kijamii, kiuchumi, na kitamaduni zinazoikabili jamii ya Watanzania.

None
None
None
None
None
None
None
None