News-Details

News >Details

WANAFUNZI WA CHUO KIKUU MZUMBE WAFANYA ZIARA YA MAFUNZO KIWANDA CHA SUKARI MKULAZI

WANAFUNZI WA CHUO KIKUU MZUMBE WAFANYA ZIARA YA MAFUNZO KIWANDA CHA SUKARI MKULAZI

Chuo Kikuu Mzumbe kupitia Skuli ya Biashara, (SoB) kimewezesha wanafunzi wa mwaka wa pili wa Shahada ya Kwanza ya Ununuzi na Mnyororo wa Usambazaji kufanya ziara ya mafunzo katika Kiwanda cha Sukari Mkulazi Holding Company, kilichopo Mbigiri, Wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro. Ziara hiyo, iliyofanyika tarehe 30 Januari 2025, chini ya mradi wa HEET, ilikuwa na lengo la kuwapa wanafunzi fursa ya kujifunza kwa vitendo⁰ mchakato mzima wa uzalishaji wa sukari, kuanzia hatua ya ununuzi wa malighafi hadi uzalishaji wa sukari. Nae, Mkuu wa Idara ya Ununuzi na Usimamizi wa Usafirishaji Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Paul Kabelele, aliongoza ziara hiyo na kuwapa wanafunzi ufafanuzi kuhusu umuhimu wa kujifunza mchakato mzima wa uzalishaji sukari kwa vitendo. Akizungumza na wanafunzi kabla ya kuingia kiwandani, Dkt. Kabelele alisisitiza kuwa fursa kama hii ni muhimu kwa kuwajengea wanafunzi uelewa wa kina kuhusu michakato ya viwanda na usimamizi wa mnyororo wa usambazaji. Aliwashauri wanafunzi kutumia nafasi hii kujifunza kwa ufanisi na kuhakikisha kuwa wanatoka na ujuzi utakaowawezesha kuwa na mchango mkubwa katika soko la ajira. Kwa upande wake, Mhandisi Deus Masala, Kaimu Mhandisi Mwandamizi Idara ya Uzalishaji katika kiwanda hicho, alieleza kuwa uzalishaji wa sukari unahitaji usimamizi makini wa ununuzi wa malighafi, uhifadhi na usindikaji wa miwa, pamoja na mifumo bora ya usambazaji ili kuhakikisha uzalishaji unafanyika kwa ufanisi. Pia alisisitiza umuhimu wa kuzingatia viwango vya ubora katika kila hatua ya mnyororo wa thamani wa sukari. Pia, Wanafunzi walipata fursa ya kujifunza kwa vitendo kwa kutembelea sehemu mbalimbali za kiwanda hicho, kujionea mashine zinazotumika katika uzalishaji wa sukari, pamoja na mifumo ya uhifadhi na usambazaji wa bidhaa. Ziara hii iliwapa wanafunzi uelewa wa kina kuhusu uhusiano kati ya nadharia wanayojifunza darasani na utekelezaji wake viwandani. Ziara hii ilikuwa ni muhimu kwa wanafunzi, kwani imewapa fursa ya kuona utekelezaji wa nadharia kwa vitendo, jambo ambalo litawaandaa vyema kwa changamoto za soko la ajira. Ni wazi kwamba mafunzo kama haya ni muhimu katika kujenga ufanisi wa wanafunzi katika taaluma yao. Mradi wa HEET umekuwa kipaumbele katika kuwezesha ziara mbalimbali, ambazo zinawasaidia wanafunzi kuongeza ufanisi wao na kujiandaa kwa njia bora zaidi katika soko la ajira.

None
None
None
None
None
None
None
None
None
None