News-Details

News >Details

BW. PRISCUS MUNGUASIFIWE AFAULU KUTETEA TASNIFU YAKE YA UZAMIVU (PhD)

BW. PRISCUS  MUNGUASIFIWE AFAULU KUTETEA TASNIFU YAKE YA UZAMIVU (PhD)

Mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) kutoka Skuli ya Biashara (SoB), Bw. Priscus Aloyce Munguasifiwe, amefanikiwa kutetea tasnifu yake kwa mafanikio makubwa. Utetezi huo umefanyika tarehe 6 Novemba 2025 katika Chuo Kikuu Mzumbe – Kampasi Kuu, Morogoro, mbele ya jopo la watahini lililoongozwa na Mwenyekiti wake Prof. Elizabeth Lulu Genda, huku Dkt. Cosmas Mbogela akiwa Msimamizi Mkuu wa Utafiti na Dkt. Joseph Kiria akiwa Msimamizi Msaidizi. Tasnifu hiyo ilijikita katika kuchambua ushawishi wa ari ya walipakodi binafsi katika kuimarisha uzingatiaji wa kodi ya mapato nchini Tanzania, kwa lengo la kuelewa sababu zinazochochea au kudhoofisha uaminifu na uwajibikaji wa walipakodi kwa mamlaka husika. Akiwasilisha utafiti wake mbele ya jopo la watahini, wanataaluma na wanafunzi wenzake, Bw. Munguasifiwe alibainisha kuwa ari chanya na maadili mema kwa walipakodi vina mchango mkubwa katika kuongeza mapato ya serikali, huku changamoto kama uelewa mdogo na ukosefu wa uwazi katika mifumo ya kodi vikitajwa kama vikwazo vinavyochangia kupungua kwa utii wa kodi. Aidha, alitoa mapendekezo kwa serikali, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), na wadau wa sekta ya kodi kuhusu mikakati ya kuelimisha walipakodi, kuongeza uwazi katika ukusanyaji wa mapato, na kuimarisha uhusiano mzuri kati ya walipakodi na mamlaka ili kuongeza morali ya ulipaji kodi. Baada ya majadiliano ya kina, Mwenyekiti wa jopo la watahini, Prof. Elizabeth Lulu Genda, alitangaza rasmi kuwa Bw. Priscus Aloyce Munguasifiwe amefaulu kutetea tasnifu yake ya Uzamivu (PhD), akisisitiza kuwa matokeo ya utafiti wake yatakuwa mchango muhimu katika kuboresha sera na mikakati ya ukusanyaji wa mapato nchini Tanzania. Hatua hii inaendeleza dhamira ya Chuo Kikuu Mzumbe katika kukuza tafiti zenye tija, ubunifu na mchango halisi katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya taifa, sambamba na kuendeleza wataalamu wabobezi wenye mchango mkubwa kwa taifa.

None
None
None
None
None
None
None