Katika kuendeleza na kukuza tafiti bunifu zinazogusa maisha ya watu na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi, Chuo Kikuu Mzumbe kimeandika historia nyingine baada ya Bw. Kernslave Wensle, mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) kutoka Taasisi ya Taaluma za Maendeleo (IDS), kufanikiwa kutetea tasnifu yake kwa mafanikio makubwa tarehe 7 Novemba 2025 katika Kampasi Kuu ya Morogoro. Utetezi huo uliongozwa na Profesa Elizabeth Lulu Genda, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa jopo la watahini, huku Dkt. Adolf Makauki akiwa msimamizi mkuu wa utafiti na Dkt. Athanas Ngalawa akiwa Msimamizi Msaidizi. Tasnifu ya Bw. Wensle yenye kichwa: “Uwajibikaji wa mamlaka za serikali za mitaa na kupunguza umaskini miongoni mwa vijana katika Jiji la Mbeya, Tanzania”, inachambua kwa undani uhusiano kati ya uwajibikaji wa mamlaka za serikali za mitaa na jitihada za kupunguza umaskini miongoni mwa vijana. Matokeo ya utafiti yanaonesha kuwa uwajibikaji wa viongozi wa serikali za mitaa una mchango mkubwa katika ustawi wa vijana, hasa kupitia usimamizi bora wa rasilimali, uwazi katika maamuzi, na ushirikishwaji wa vijana katika miradi ya maendeleo. Aidha, Bw. Wensle alipendekeza kuimarishwa kwa mifumo ya uwazi na uwajibikaji ili kuongeza ufanisi wa sera za kupunguza umaskini katika ngazi za chini za utawala. Baada ya majadiliano ya kina, Profesa Genda alimtangaza rasmi Bw. Kernslave Wensle kuwa amefaulu kutetea tasnifu yake ya Uzamivu, akisisitiza kuwa utafiti huo umechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza uelewa kuhusu uhusiano kati ya utawala bora na maendeleo ya vijana nchini. Mafanikio haya yanaonesha jinsi Chuo Kikuu Mzumbe kinavyosukuma mbele malengo yake ya kuwa kitovu cha tafiti zenye mchango wa kweli katika maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla, huku Taasisi ya Taaluma za Maendeleo (IDS) ikithibitisha nafasi yake kama nguzo muhimu ya maarifa ya kijamii na kiuchumi.