News-Details

News >Details

LAZARO MWONGE AFANIKIWA KUTETEA TASINIFU YAKE YA UZAMIVU CHUO KIKUU MZUMBE

LAZARO MWONGE AFANIKIWA KUTETEA TASINIFU YAKE YA UZAMIVU CHUO KIKUU MZUMBE

Katika hatua muhimu inayothibitisha ubunifu na tija ya tafiti za kisayansi zinazochangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi, Bw. Lazaro Mwonge, mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) kutoka Kitivo cha Sayansi za Jamii (FSS) Chuo Kikuu Mzumbe, ameibuka kidedea baada ya kufanikisha kwa mafanikio utetezi wa tasnifu yake leo tarehe 7 Novemba 2025, katika Kampasi Kuu ya Morogoro. Utetezi huo umefanyika mbele ya Profesa Emmanuel Ndikumana, Mwenyekiti wa jopo la watahini, huku Prof. Charles Tundui akiwa msimamizi mkuu na Dkt. Robert Lihawa akiwa msimamizi msaidizi katika mchakato mzima wa utafiti. Tasnifu ya Bw. Mwonge yenye kichwa: “Upatikanaji na matumizi ya mikopo midogo: athari zake kwa uzalishaji wa kilimo kwa wakulima wadogo nchini Tanzania” inachambua jinsi mikopo midogo inavyoweza kuongeza uzalishaji wa kilimo, kuboresha kipato cha kaya, na kuimarisha ustawi wa jamii za vijijini. Utafiti huo pia umebainisha changamoto zinazowakabili wakulima, ikiwemo masharti magumu ya mikopo, ukosefu wa dhamana, na uelewa mdogo wa kifedha. Baada ya utetezi, Bw. Mwonge alijibu maswali kutoka kwa jopo la watahini, akifafanua mbinu alizotumia kupata matokeo yake na kueleza jinsi mapendekezo yake yanavyoweza kusaidia kuongeza ufanisi wa mikopo midogo nchini. "Utafiti huu unaonesha jinsi mikopo midogo inaweza kuwa chachu ya maendeleo vijijini, na nina matumaini kwamba mapendekezo yake yatachangia katika kuboresha hali ya wakulima wadogo nchini." Alisema bw. Mwonge. Naye Mwenyekiti wa jopo la watahini, Profesa Emmanuel Ndikumana, alimsifu Bw. Mwonge kwa kuonesha umahiri wa hali ya juu katika kuwasilisha matokeo na kujibu maswali kwa kina, akibainisha kuwa utafiti huu una mchango mkubwa katika kuboresha mifumo ya mikopo na kuongeza tija ya kilimo nchini. Mafanikio haya yanathibitisha dhamira ya Chuo Kikuu Mzumbe katika kukuza tafiti bunifu zenye tija kwa jamii na kuchangia maendeleo endelevu ya taifa.

None
None
None
None
None
None
None