News-Details

News >Details

MKUU WA CHUO MZUMBE DKT. SHEIN APOKEA TAARIFA YA MAANDALIZI YA MAHAFALI YA 24

MKUU WA CHUO MZUMBE DKT. SHEIN APOKEA TAARIFA YA MAANDALIZI YA MAHAFALI YA 24

Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe ambaye pia ni Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti Mstaafu wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein, amepokea taarifa ya maandalizi ya Mahafali ya 24 ya Chuo Kikuu Mzumbe iliyowasilishwa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. William Mwegoha, leo Nov. 15, 2025 jijini Dar es Salaam. Prof. Mwegoha ameeleza kuwa maandalizi yanaendelea kwa kiwango cha kuridhisha na kubainisha kuwa jumla ya wanachuo 5,091 wanatarajiwa kuhitimu ngazi mbalimbali za kitaaluma kutoka Kampasi Kuu Morogoro, Ndaki ya Mbeya na Ndaki ya Dar es Salaam. Pia, Prof. Mwegoha aliongeza kuwa maandalizi yamejikita katika kuboresha na kuhakikisha mazingira ya chuo yanaakisi hadhi ya tukio, ambalo ni miongoni mwa matukio makubwa ya kitaaluma yanayovuta hisia za jamii na wadau wa elimu nchini. Aidha, Prof. Mwegoha alimweleza Mkuu wa Chuo kuhusu Mkutano wa Baraza la Wahitimu utakaofanyika tarehe 19 Novemba 2025 katika Kampasi Kuu Morogoro, ambapo Mhe. Philemon Luhango, Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu, ndiye atakayekuwa Mgeni Rasmi. Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo, Dkt. Shein aliipongeza Baraza na Menejimenti ya Chuo kwa maandalizi ya kuridhisha na kueleza kufurahishwa kwake na kuongezeka kwa idadi ya wahitimu mwaka huu, sambamba na uwiano mzuri wa kijinsia, ambapo takwimu zinaonesha asilimia 53 ni wanawake na 47 ni wanaume. Alisema ongezeko hilo linaonesha utekelezaji mzuri wa sera za ujumuishaji, usawa wa kijinsia na ubora wa elimu inayotolewa na chuo. Kwa msisitizo, Dkt. Shein amewataka wahitimu kuhudhuria mahafali na kuthamini heshima waliyopewa ya kuhitimu katika taasisi yenye historia kama Mzumbe. Ameeleza kuwa mahafali ni tukio la kujitambulisha kwa jamii kama wasomi walio tayari kuchukua nafasi zao kwenye taifa.

None
None
None
None
None
None
None
None