Chuo Kikuu Mzumbe kimeendelea kupanua wigo wa kujenga uwezo katika Uongozi na Usimamizi wa Sekta ya Afya kupitia mafunzo kwa Waganga Wafawidhi wa Wilaya, yaliyofunguliwa leo katika Hoteli ya Edema, Morogoro. Uzinduzi wa mafunzo haya umefanywa na mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Bw. Issa Ng’imba, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu. Mafunzo haya yanawahusisha zaidi ya washiriki 90 kutoka mikoa mbalimbali nchini na yanafanyika kuanzia tarehe 17 hadi 21 Novemba 2025, yameandaliwa na Kituo cha Umahiri cha Ufuatiliaji na Tathmini ya Afya (CoE-HME) cha Chuo Kikuu Mzumbe kwa ushirikiano na Wizara ya Afya na Global Fund. Bw. Ng’imba ameeleza kuwa Serikali imeendelea kuimarisha mifumo ya afya, lakini ufanisi wake unategemea kwa kiasi kikubwa utendaji wa viongozi walipo ngazi ya wilaya na vituo vya afya. “Haya mafunzo yanakuja wakati muafaka. Tunahitaji viongozi wa afya wanaoongoza na kusimamia rasilimali kwa uadilifu, na wanaoweka matakwa ya wananchi mbele ya maslahi binafsi,” alisema. Aliongeza kuwa Wizara inatarajia washiriki kutumia mafunzo hayo kuboresha upangaji wa huduma, menejimenti ya rasilimali watu, na ufuatiliaji wa huduma za afya. Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha, alishukuru Wizara kwa kuendelea kukiamini Chuo hicho katika kuandaa viongozi wa afya nchini. “Kupata jukumu hili kwa mara ya pili ni heshima kwa Mzumbe. Tunaendelea kuboresha mitaala yetu ili iendane na changamoto halisi zinazowakabili viongozi wa afya nchini,” alisema Prof. Mwegoha. Awali, Mratibu wa Miradi ya Afya wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. Henry Mollel, alisema mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati mpana wa taifa katika kuimarisha mifumo ya afya kupitia tathmini iliyofanywa wakati wa maandalizi ya Global Fund. Pia, Prof. Mollel alieleza kuwa tofauti na programu nyingine, mara hii washiriki watapitishwa katika mpango wa ufuatiliaji baada ya mafunzo ili kupima mabadiliko na athari za mafunzo katika maeneo yao ya kazi. Mafunzo hayo yanatarajiwa kuleta mabadiliko chanya katika ngazi ya wilaya kwa kuwawezesha viongozi wa afya kusimamia kwa ufanisi rasilimali za afya, kuongeza uwajibikaji, na kuboresha huduma kwa wananchi, sambamba na dira ya Serikali ya kuboresha huduma za afya kote nchini.