Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Philemon Luhanjo, amewataka wahitimu wa Chuo Kikuu Mzumbe kuendelea kuwa mabalozi bora wa chuo hicho kwa kutumia maarifa na ujuzi walioupata wakati wa masomo yao. Mhe. Luhanjo amesema hayo tarehe 19 Novemba 2025 wakati wa Mkutano wa 25 wa Baraza la Wahitimu uliofanyika Chuo Kikuu Mumbe Kampasi Kuu, Morogoro na kuhudhuriwa na wahitimu, viongozi wa Chuo pamoja na wadau mbalimbali ambapo alisisitiza umuhimu wa wahitimu kuendeleza maadili, uadilifu na uzalendo katika maeneo yao ya kazi ili kuchochea maendeleo ya taifa. Aidha, aliwataka wanafunzi na wahitimu kuwa na imani na Chuo Kikuu Mzumbe huku akisisitiza kuwa Chuo hicho kimekuwa kikitengeneza watawala wa ngazi za juu katika maeneo ya utawala, sheria na biashara. “Chuo kimetoa viongozi wa kitaaluma, na wahitimu wake wamepikwa vizuri hata Rais wa Jamhuri na Makamu wake ni wahitimu wa Chuo hiki. Sio Chuo kidogo, nanyi sio wadogo,” alisisitiza Mhe. Luhanjo. Akiongea kwa niaba ya Rais wa Baraza la Wahitimu CPA Ludovick Utouh, Makamu Mkuu wa Chuo, Prof William Mwegoha alisisitiza juu ya umuhimu wa wahitimu kuendeleza ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira na kuongeza kuwa ushirikiano kati ya chuo na wahitimu ni muhimu katika kuboresha programu za masomo, miundombinu na maendeleo endelevu. “Baraza hili ni fursa ya kuimarisha uhusiano kati ya Chuo na wahitimu wake, ambao ni mabalozi wetu katika jamii. Tunategemea mchango wenu katika kufanikisha malengo endelevu ya Chuo Kikuu Mzumbe,” alisema Prof. Mwegoha. Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri, Prof. Hawa Tundui alieleza kuhusu umuhimu wa wahitimu kushirikiana na Chuo katika miradi ya maendeleo, tafiti na machapisho ya kitaaluma. Aliushukuru uongozi wa Chuo, wahitimu na wadau kwa michango yao, ikiwemo ya CRDB na BRELA, akibainisha kuwa misaada hiyo inaendelea kuhamasisha wahitimu kushiriki kikamilifu katika shughuli za Chuo. Naye, Mkurugenzi wa Kitengo cha Ukimataifaji na Baraza la Wahitimu Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Lucy Massoi aliwasilisha mipango ya Baraza hilo kwa mwaka huu ikiwemo kuimarisha mfuko wa kudumu wa michango ya wahitimu (Endorsement Fund) kuboresha matumizi ya teknolojia, na kuendeleza taswira bora ya Chuo kupitia machapisho ya mara kwa mara kwenye majukwaa ya kimataifa mtandaoni. Mkutano huo pia ulihusisha utoaji wa tuzo kwa wanafunzi bora, huku Baraza la Wahitimu likitangaza mpango wa kuwasaidia wanafunzi wahitaji kupitia ufadhili na udhamini wa masomo (scholarship na sponsorship). Wanafunzi wawili watafadhiliwa moja kwa moja kupitia Mfuko wa kudumu wa michango ya wahitimu (Endorsement Fund) na wengine wawili kupitia taasisi ya mmoja wa wahitimu wa Chuo Kikuu Mzumbe, na kufanya jumla ya wanafunzi wanne watakaopokea msaada wa kifedha kuendeleza masomo yao.