News-Details

News >Details

MZUMBE YATAMATISHA MAFUNZO YA UONGOZI KWA WAGANGA WAFAWIDHI, MKAZO KATIKA UBORESHAJI WA HUDUMA ZA AFYA

MZUMBE YATAMATISHA MAFUNZO YA UONGOZI KWA WAGANGA WAFAWIDHI, MKAZO KATIKA UBORESHAJI WA HUDUMA ZA AFYA

Mafunzo ya Uongozi na Usimamizi wa Sekta ya Afya kwa Waganga Wafawidhi wa Wilaya, yaliyoandaliwa na Chuo Kikuu Mzumbe kupitia Kituo cha Umahiri cha Ufatiliaji na Tathmini ya Afya (COEHME - SoPAM), yamefungwa rasmi tarehe 21 Novemba 2025 katika Hoteli ya Edema mkoani Morogoro, yakibeba ujumbe wa mageuzi na maboresho ya mifumo ya afya katika ngazi ya msingi. Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Mgeni Rasmi ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI (Afya) Prof. Tumaini Nagu, alikipongeza Chuo Kikuu Mzumbe kwa kuendelea kuwa mshirika thabiti wa Serikali katika kujenga uwezo wa viongozi wa afya. Amesema uamuzi wa Chuo kuendesha mafunzo haya nje ya majukumu yake ya kawaida ya kitaaluma ni ishara ya uzalendo na kujituma katika kutimiza wajibu wa kijamii. Aidha, Prof. Nagu aliwakumbusha Waganga Wafawidhi kwamba dhamana waliyonayo ni kubwa, na matokeo ya huduma za afya kwa wananchi yanategemea maamuzi yao ya kila siku. Aliwasisitiza kutumia maarifa waliyopata kuboresha utendaji, kusimamia ipasavyo rasilimali, kuimarisha nidhamu ya watumishi na kufanya maamuzi yanayotumia takwimu. “Taifa linawatazama kama injini ya mageuzi katika sekta ya afya; hivyo, rudi kwenye vituo vyenu kwa kasi mpya, ubunifu na moyo wa kuwahudumia wananchi,” alisema Prof. Nagu. Awali, Prof. Henry Mollel, Mratibu wa Miradi ya Afya wa Chuo Kikuu Mzumbe ambaye pia ni Rasi wa Ndaki ya Mbeya, alisema mafunzo hayo yamejengwa kwa kuzingatia changamoto halisi zinazojitokeza katika utendaji wa sekta ya afya. Amesisitiza kuwa pasipo uongozi thabiti, ni vigumu kutekeleza sera na afua za afya kwa matokeo chanya. Aliongeza kuwa mafunzo hayo ya siku tano yenye moduli 15 ya msingi yametoa ujuzi muhimu kwa Waganga Wafawidhi wanaosimamia vituo 87 nchini, na hivyo kuleta matumaini mapya ya maboresho katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi. Kwa upande wake Dkt. Paul Chaote, Mkurugenzi Msaidizi – Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), alilitaja darasa hilo kuwa sehemu muhimu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha uongozi na usimamizi wa huduma katika ngazi ya halmashauri. Alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuongeza fursa za mafunzo ili kuhakikisha viongozi wa afya wanapata maarifa ya kisasa yanayohitajika katika zama hizi za mabadiliko ya kimfumo. Vilevile, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Best Magoma alieleza kuwa ujuzi waliopata hasa katika uongozi, matumizi ya takwimu, usimamizi wa rasilimali na kupanga mikakati, utakuwa chachu ya maboresho ya huduma na kupunguza malalamiko kutoka kwa wananchi. Naye Prof. Gabriel Komba, Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma, Utafiti na Ushauri, alisisitiza kuwa Chuo kitaendelea kuwa kitovu cha kutoa viongozi wa afya wenye maono, weledi na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi. Alisema mafunzo hayo yametekelezwa kwa mbinu shirikishi na kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa afya, hatua inayothibitisha dhamira ya Chuo ya kuendeleza elimu na utafiti unaochochea maendeleo ya Taifa. Chuo Kikuu Mzumbe kitaendelea kuthibitisha nafasi yake kama kitovu cha utaalamu wa menejimenti ya afya, na itaendelea kuunga mkono jitihada za kujenga ngazi ya msingi yenye ufanisi na inayoweka mahitaji ya mwananchi mbele. Kupitia ujuzi, mbinu na stadi za uongozi walizopata Waganga Wafawidhi, itaweka msingi imara wa mageuzi endelevu yanayolenga kuinua ustawi wa jamii na kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora, za haki na zenye tija. Huu ni mwendelezo wa kuakisi kaulimbiu yake Chuo hicho: “ Tujifunze kwa maendeleo ya watu”.

None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None