Rasi wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Mbeya, Prof. Henry Mollel amekutana na kuzungumza na watumishi wa Ndaki hiyo katika ukumbi wa Nkurumah Chuoni hapo tarehe 28 Novemba 2025, mkutano huo ulilenga kujadili uwajibikaji, kutoa mrejesho wa utekelezaji wa majukumu ya Ndaki ya Mbeya, pamoja na kutoa maelekezo na mwelekeo wa pamoja katika kufika malengo ya Chuo kama ilivyo kwenye Mpango Mkakati wa Chuo Kikuu Mzumbe. Akifungua mkutano huo, Prof. Mollel aliwashukuru wafanyakazi wote kwa mchango wao mkubwa katika kutekeleza na kufanikisha majukumu ya Chuo, hasa katika kipindi cha mwaka wa masomo wa 2024/2025. Huku akisisitiza juu ya umuhimu wa mshikamano, uwajibikaji, na mawasiliano yenye tija miongoni mwa watumishi. “Mafanikio yoyote ya taasisi yanatokana na ushirikiano wa dhati kati ya uongozi na wafanyakazi. Ndiyo maana tunakutana leo kusikilizana, kutafakari tulipotoka, tulipo na tunapokwenda ili kuweka malengo na mipango madhubuti ya mbele kwa pamoja,” alisema Prof Mollel. Vilevile, Rasi wa Ndaki hiyo alitoa pongezi za dhati kwa watumishi na kamati ya maandalizi ya Sherehe ya Mahafali ya 24 ya Ndaki ya Mbeya kwa kuratibu na kufanikisha sherehe hiyo kwa ubora. Aidha katika mkutano huo, mambo mbalimbali yalijadiliwa yakiwemo masuala ya ushirikiano na mshikamano baina ya watumishi, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu, maendeleo ya watumishi, miradi inayotekelezwa chuoni, uboreshaji wa mazingira ya kazi, mashirikiano na ukimataifaji pamoja na huduma bora kwa wateja. Nao watumishi wa Ndaki ya Mbeya walipata wasaa wa kuuliza maswali na kutoa maoni juu ya utekelezaji wa majukumu yao ili kuendelea kuleta chachu ya uwajibikaji, ushirikiano na maendeleo binafsi na ya taasisi kwa ujumla. Mkutano huo umeonekana kuwa wa muhimu katika kudumisha mahusiano na mawasiliano kati ya uongozi na watumishi wa Ndaki ya Mbeya, na imeshauriwa mikutano ya namna hiyo iwe ni utamaduni endelevu ya Chuo Kikuu Mzumbe ili kuendelea kukumbushana na kuelekezana juu ya masuala muhimu ya kiutumishi.