News-Details

News >Details

KAMATI YA UENDESHAJI WA MRADI WA HEET YAKAGUA UJENZI NDAKI YA TANGA

KAMATI YA UENDESHAJI WA MRADI WA HEET YAKAGUA UJENZI NDAKI YA TANGA

Kamati ya Uendeshaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) Chuo Kikuu Mzumbe imefanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa ndaki mpya ya Tanga. Ziara hiyo iliongozwa na Naibu Mratibu wa Mradi wa HEET Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. Hawa Tundui, ambaye alisema kuwa kamati imefanya ukaguzi wa kina wa miradi ya majengo yanayojengwa na kuhakikisha kuwa mradi unakwenda vizuri kwa kasi inayotarajiwa. Prof. Tundui alisema, “Nashukuru mkandarasi kwa juhudi zake. Anaendelea vizuri na kwa asilimia aliyofikia, majengo mengi yameanza kuonekana wazi. Kwa sasa mradi umefikia asilimia zaidi ya 30, na kwa kasi anayoiweka, anaweza kufikia mwisho wa mradi kama ilivyopangwa mwezi Desemba mwaka huu.” Aidha, Prof. Tundui alitaja changamoto zinazoweza kukumba mradi, ikiwa ni pamoja na mvua zinazotarajiwa kunyesha siku zijazo. “Tumemshauri mkandarasi ahakikishe kuwa vifaa vyote vipo kwenye eneo la ujenzi ili mvua isiwe kikwazo kikubwa katika kufanikisha mradi kwa wakati,” aliongeza. Awali, Mhandisi Lucas Maganga, Msimamizi wa Ujenzi kutoka kampuni ya Dimetoclasa Real Hope Limited, alisema kuwa ujenzi wa ndaki ya Tanga unaendelea kwa kasi na ubora unaotakiwa. Alibainisha kuwa kwa sasa, mradi umeifikia asilimia 36 kwa Lot 1 (jengo la masomo, mgahawa na kituo cha afya) na asilimia 38 kwa Lot 2 (hosteli za wanafunzi, nyumba za wafanyakazi na mifumo ya maji safi na maji taka). Kwa upande wake, Msimamizi wa Ujenzi wa Ndaki ya Tanga, Bw. Prosper Leonard alisema kuwa wajumbe wa kamati wamefurahishwa na kasi ya ujenzi inayofanywa na mkandarasi. “Kuna baadhi ya majengo ambayo yameendelea kwa kasi sana, na tumemsisitiza mkandarasi kuzingatia ubora wa kazi wakati wa ujenzi,” alisema Bw. Leonard. Pia, aliongeza kuwa ukaguzi unaoendelea kufanywa unahusisha kuhakikisha kuwa vifaa vyote vinavyotumika kwenye ujenzi vina viwango vya hali ya juu na vinakidhi vigezo vilivyowekwa. Ujenzi huo wa Ndaki ya Tanga unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba mwaka huu na utasaidia kuboresha miundombinu ya elimu kwa kuongeza wigo wa upatikanaji wa elimu nchini.

None
None
None
None
None
None
None