News-Details

News >Details

RASI WA NDAKI YA MBEYA AKUTANA NA KUZUNGUMZA NA WANAFUNZI

RASI WA NDAKI YA MBEYA AKUTANA NA KUZUNGUMZA NA WANAFUNZI

Rasi wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Mbeya, Prof. Henry Mollel amefanya mkutano maalumu na wanafunzi wa mwaka wa kwanza kwa mwaka wa masomo 2025/2026, uliofanyika katika Ukumbi wa Nkurumah, Ndaki ya Mbeya tarehe 28 Novemba, 2025 kwa lengo la kuwakaribisha rasmi Chuoni na kuwaelekeza kuhusu wajibu wao kama wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe. Katika hotuba yake, Prof. Henry Mollel aliwataka wanafunzi hao kuzingatia nidhamu, maadili, na bidii katika masomo, akibainisha kuwa mambo hayo ni ya msingi kwa mafanikio ya kitaaluma na ya baadaye. Alisisitiza kuwa chuo ni mahali pa kujenga msingi wa maisha, hivyo kila mwanafunzi anatakiwa kuwa makini na muda wake, kuchagua marafiki sahihi na kuepuka vishawishi. “Mnayo nafasi ya kipekee kujenga mustakabali wenu. Hakikisheni mnatumia kila fursa kujifunza, kujiboresha na kuchangia maendeleo ya taifa. Zingatieni miongozo, sheria na kanuni za chuo – maana ndizo zinazoongoza maisha yenu ya kila siku hapa chuoni,” alisema Prof. Mollel. Naye, Naibu Rasi wa Ndaki ya Mbeya, Prof. Charles Tundui aliwakumbusha wanafunzi hao kuhusu kusoma kwa bidii kwani hilo ndio lengo kuu lililowaleta Chuoni. “Umekuja Chuoni kusoma na kujifunza na sio kucheza. Kuna msemo ulivuma kipindi cha nyuma unasema, graduate with A’s not with AIDS’, hivyo basi muwe makini,” alisema Prof. Tundui. Aidha, mkutano huo ulieleza kuhusu miradi mikubwa ya kuboresha mazingira ya usalama na ujifunzaji kama vile mradi wa Zahanati ya Ndaki ya Mbeya uliogharimu shilingi milioni 465,706,251.70 na sasa Zahanati hiyo inatoa huduma kwa wote. Hivyo, Wanafunzi watanufaika na huduma bora na za haraka za afya ndani ya Chuo. Viongozi wa idara na vitengo mbalimbali pia walipata nafasi ya kuzungumza, wakitoa maelezo kuhusu huduma zinazopatikana chuoni, ikiwa ni pamoja na idara za kitaaluma, kitengo cha huduma kwa wanafunzi, TEHAMA, Maktaba, Udahili na Fedha. Vilevile, Prof. Mollel alitoa maelekezo kwa ofisi husika zinazosimamia ukarabati wa miundombinu ya Chuo kukamilika haraka iwezekanavyo. Wanafunzi waliuliza maswali na kutoa maoni yao kuhusu taratibu na miongozo mbalimbali ya Chuo, huku wakionesha shauku kubwa ya kuanza safari yao ya kitaaluma. Wanafunzi wengi walieleza kufurahishwa na mapokezi mazuri na mkutano huo wa wazi, wakisema umewasaidia kuelewa vizuri matarajio ya Chuo kwao na wajibu wao binafsi katika kujenga maisha yao ya baadaye. Mkutano huo ulihitimishwa kwa wito wa ushirikiano baina ya wanafunzi na uongozi wa Chuo, huku wakihimizwa kutumia muda wao vizuri, kufuata sheria za Chuo na kuwa na nidhamu bora.

None
None
None
None
None
None
None
None