News-Details

News >Details

MZUMBE YAICHARAZA BOT KATIKA MPIRA WA WAVU SHIMMUTA 2025

MZUMBE YAICHARAZA BOT KATIKA MPIRA WA WAVU SHIMMUTA 2025

Timu ya mpira wa wavu kwa wanaume kutoka Chuo Kikuu Mzumbe imeibuka mshindi baada ya kuicharaza timu ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kwa seti 2–0 katika Mashindano ya Shirikisho la Michezo la Mashirika ya Umma, Taasisi na Makampuni Binafsi Tanzania (SHIMMUTA) 2025 yanayoendelea katika viwanja mbalimbali mkoani Morogoro. Nahodha wa timu hiyo, Dkt. Lukiko Lukiko, amewapongeza wachezaji wake kwa ushindani na ari waliyoionesha, akibainisha kuwa mashindano ya SHIMMUTA yameandaliwa kwa lengo la kuimarisha afya, ushirikiano na umoja kwa watumishi. Chuo Kikuu Mzumbe kinashiriki kupitia timu za mpira wa wavu, mpira wa miguu, riadha, bao, pool table na karata. “Tumejipanga vizuri, wachezaji wana nidhamu na nguvu ya kupambana hadi mwisho. Lengo letu ni kuhakikisha Mzumbe inarejea na makombe mwaka huu. Tumekuja kwa kasi,” alisema Dkt. Lukiko. Kwa upande wa soka, Mzumbe ilianza kwa sare ya 1–1 dhidi ya Bohari ya Dawa (MSD), kabla ya kukutana na BOT leo na kukubali kichapo cha mabao 3–0. Hata hivyo, benchi la ufundi linaendelea kurekebisha mapungufu kuelekea mechi zijazo za hatua ya makundi. Mashindano ya SHIMMUTA 2025 yanaendelea kutimua vumbi, huku Chuo Kikuu Mzumbe kikiendelea kupambana kuhakikisha kinafanya vizuri na kurejea na mafanikio katika michezo mbalimbali.

None
None
None
None
None
None
None
None