News-Details

News >Details

DKT. SHEIN AONGOZA SHEREHE ZA MAHAFALI YA CHUO KIKUU MZUMBE NDAKI YA DAR ES SALAAM

DKT. SHEIN AONGOZA SHEREHE ZA MAHAFALI YA CHUO KIKUU MZUMBE NDAKI YA DAR ES SALAAM

Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Ali Mohamed Shein ambaye ni Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mwenyekiti Mstaafu wa Baraza za Mapinduzi ya Zanzibar , amewataka wahitimu wa Ndaki ya Dar es Salaam kujenga mitandao imara ya kitaaluma na kutumia maarifa yao kutambua fursa halali zilizopo katika mazingira mapana ya kiuchumi na kijamii. Akizungumza leo katika mahafali ya 24 yaliyofanyika Mlimani City Jijini Dar es Salaam, amesema mafanikio ya kitaaluma yanahitaji juhudi binafsi na uwezo wa kujenga uhusiano unaofungua milango ya maendeleo. Dkt. Shein amesema baadhi ya wanafunzi wa sheria wa Chuo hicho waliopata nafasi ya kushiriki mashindano ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (Moot Court) nchini Austria ni ushahidi kuwa mitandao ya kitaaluma huongeza maarifa na fursa. “Mashindano kama haya yanawakutanisha wanafunzi kutoka duniani kote na ni nafasi ya kujifunza taaluma, mila na utamaduni. Hapa ndipo msingi wa kujenga mitandao ya uhusiano katika taaluma zenu,” amesema Dkt. Shein. Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Prof. Saida Yahaya Othman, amesisitiza umuhimu wa maadili, uadilifu, uwajibikaji na kujifunza endelevu katika safari ya wahitimu. Amesema msingi wa elimu bora ni uwezo wa kuibadilisha jamii, kujifunza kutoka kwa kila mtu hata yule asiye na elimu huku akisisitiza kauli mbiu ya Chuo Kikuu Mzumbe “Tujifunze kwa maendeleo ya watu.” Naye Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. William Mwegoha, amesema Ndaki hiyo ina jumla ya wanafunzi 1,793, wakiwemo 939 wanawake na 854 wanaume, hali inayodhihirisha ongezeko la mwitikio wa wanafunzi wa kike kujiendeleza kielimu. Ameeleza pia kuwa Ndaki imeendelea kutoa huduma kwa jamii kupitia semina za uelewa wa sheria kwa wanawake wa Tegeta, mafunzo ya biashara kwa wajasiriamali wa Ice Cream, na elimu ya maktaba mtandao kwa wanafunzi wa sekondari. Prof. Mwegoha ameongeza kuwa Chuo kinaendelea kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia, ikiwemo maboresho ya TEHAMA, ujenzi wa viwanja vya michezo, ukarabati wa majengo na ujenzi wa jengo la taaluma Tegeta lenye thamani ya shilingi bilioni 4.8 ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 15.Sambamba na hayo Prof. Mwegoha amemueleza mkuu wa chuo juu ya kuanzishwa kwa programu ambapo katika mwaka wa masomo 2025/2026 Ndaki imeanzisha program mpya ikiwemo Astashahada ya Uhasibu, Stashahada ya Uhasibu , Stashahada katika Menejimenti ya Biashara pamoja na Shahada ya Awali ya Menejimenti ya Rasilimali Watu . Ikumbukwe kuwa Katika Mahafali haya ya Chuo Kwa Ndaki ya Dar es Salaam jumla ya wanachuo 752 wametunukiwa stahiki zao katika ngazi mbalimbali za kitaaluma. Katika hao, wahitimu 560 wametunukiwa Shahada za Umahiri, na kati ya hao wanaume ni 251 sawa na asilimia 44.8 na wanawake 309 sawa na asilimia 55.18. Wahitimu 192 wametunukiwa Shahada ya Kwanza/awali, kati ya hao 82 sawa na asilimia 43 ni wanawake na 110 sawa na asilimia 57 ni wanaume.

None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None