Chuo Kikuu Mzumbe kinaendelea kuimarisha utoaji wa elimu na uendeshaji wa shughuli za kiutawala kupitia mafunzo ya mifumo mipya ya kidijitali iliyobuniwa chini ya Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET). Mafunzo hayo yamefanyika kuanzia tarehe 15 hadi 16 Desemba 2025 katika Hoteli ya Morena, Morogoro, yakihusisha viongozi wa kitaaluma na wakuu wa idara kutoka kampasi kuu Mzumbe pamoja na ndaki za Dar es Salaam na Mbeya. Akifungua mafunzo hayo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha, alisema matumizi ya mifumo ya kidijitali ni hatua muhimu katika kuendana na kasi ya maendeleo ya teknolojia na kuboresha ufundishaji, usimamizi wa masomo, na utoaji wa huduma za kiutawala. Aliwahimiza washiriki kuhakikisha wanapata uelewa wa kina wa mifumo hiyo ili kuongeza ufanisi, uwazi na ubora wa huduma chuoni. Kwa upande wake, Mratibu wa mradi wa HEET, Prof. Hawa Tundui, alisema mradi huo unalenga kupanua upatikanaji wa elimu ya juu na kuboresha mifumo ya kidijitali ili kuwawezesha wanafunzi kusoma kwa ufanisi popote walipo nchini. Aliongeza kuwa kwa mwaka wa masomo 2025/2026, Chuo Kikuu Mzumbe kimeanzisha programu za masomo kwa mfumo mseto (blended learning) ili kuendana na mahitaji ya soko la ajira. Naye Mratibu wa HEET upande wa mifumo ya kidijitali, Dkt. Mohamed Ghasia, alisema mafunzo hayo yamelenga kutoa uelewa wa vitendo kuhusu matumizi ya mifumo mipya, ikiwemo maboresho ya mifumo ya maktaba, TEHAMA, MU-ARMS, mtandao wa intaneti, pamoja na upatikanaji wa vitabu vya programu na vifaa kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum. Mafunzo hayo yaliendeshwa na mtaalamu wa TEHAMA, Bw. Senzota Kivaria, aliyewaongoza washiriki kufahamu mifumo mipya iliyoundwa, mazoezi ya vitendo na majadiliano, hatua iliyowawezesha kupata ujuzi wa moja kwa moja wa matumizi ya mifumo hiyo katika majukumu yao ya kila siku.