Chuo Kikuu Mzumbe kimefanya Warsha ya Uhakiki wa Mtaala wa programu mpya ya Stashahada ya Uzamili chini ya Mradi wa Kuendeleza Ubunifu wa Kijamii na Ujasiriamali kupitia Mafunzo ya Umahiri (ADVANCE Project), wenye lengo la kukuza ubunifu wa kijamii na ujasiriamali wa vitendo unaojibu mahitaji ya jamii na soko la ajira. Warsha hiyo ilifanyika tarehe 19 Desemba 2025, Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi Kuu - Morogoro na iliwakutanisha wadau mbalimbali ili kutoa maoni yatakayosaidia kuboresha mtaala unaoandaliwa. Akifungua warsha hiyo, Kaimu Mratibu wa Mradi wa ADVANCE, Dkt. Nsubili Isaga, alisema zoezi hilo ni hatua muhimu ya awali ya kukusanya mapendekezo ya kitaalamu kwa lengo la kuwawezesha wanafunzi kutambua na kutatua changamoto za kijamii kupitia ujasiriamali unaozingatia ushahidi, usawa wa kijinsia na athari endelevu kwa jamii. Kwa upande wake, Mhadhiri Msaidizi wa Idara ya Uchumi na muwezeshaji wa warsha, Bw. James Marandu, aliwasilisha hatua zilizokwishafanyika katika maandalizi ya programu hiyo, akieleza kuwa inalenga kuwajengea wanafunzi uwezo wa kujiajiri na kuanzisha miradi ya kijamii yenye tija, badala ya kuwaandaa tu kwa ajira rasmi. Washiriki wa warsha walijadili kwa kina muundo wa mtaala, ikiwemo mihula ya masomo, masomo ya lazima, mfumo wa tathmini unaozingatia viwango vya kimataifa, pamoja na umuhimu wa kujumuisha masomo ya fedha, sheria, ubunifu na utafiti. Pia walisisitiza matumizi ya mbinu shirikishi za ufundishaji zitakazomwezesha mwanafunzi kupata uzoefu wa moja kwa moja katika jamii. Mradi wa ADVANCE unatekelezwa kwa ushirikiano wa washirika 10, wakiwemo vyuo vikuu saba kutoka Tanzania, Uganda na Ulaya, pamoja na taasisi tatu zisizo za kielimu. Chuo Kikuu Mzumbe kinatarajia mtaala huu mpya kuzalisha wahitimu wenye ujuzi wa vitendo, ubunifu na mtazamo wa ujasiriamali, watakaoweza kuanzisha na kuendeleza miradi yenye mchango chanya wa kijamii na kiuchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki.