Chuo Kikuu Mzumbe kimewajengea ujuzi wa kitaaluma na vitendo wanafunzi wa mwaka wa pili wa Shahada ya Ununuzi na Usimamizi wa Mnyororo wa Usambazaji kupitia ziara ya mafunzo ya siku moja iliyolenga kujifunza kuhusu Usimamizi wa Mali za Serikali na Umma, iliyofanyika tarehe 15 Disemba 2025 katika Wizara Fedha jijini Dodoma. Ziara hiyo iliwakutanisha wanafunzi, wahadhiri na wataalamu wa Wizara ya Fedha ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha elimu inayozingatia vitendo na mahitaji ya soko la ajira. Mafunzo yalifunguliwa na Mkurugenzi wa Usimamizi wa Mali za Serikali, Bw. Chotto Sendo, ambaye alieleza kuwa Wizara ya Fedha imejipanga kuwajengea wanafunzi uelewa wa sera, sheria na mifumo ya usimamizi wa mali za umma, akisisitiza umuhimu wa uwajibikaji na matumizi bora ya rasilimali za umma. Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Ununuzi na Ugavi wa Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Paul Nsimbila, amesema mafunzo hayo yamelenga kuwaunganisha wanafunzi na mazingira halisi ya utekelezaji wa majukumu ya ununuzi na usimamizi wa mali za umma ili kuoanisha nadharia na vitendo. Aliongeza kuwa chuo kipo katika hatua za mwisho za kusaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) na Wizara ya Fedha ili kuwezesha mafunzo ya kitaalamu, ziara za kielimu na programu za kujengeana uwezo. Mafunzo yalifungwa na Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu wa Wizara hiyo Bw. Lusius R. Mwenda, ambaye alipongeza Chuo Kikuu Mzumbe kwa kuanzisha programu ya Shahada ya Ununuzi na Usimamizi wa Mali, akibainisha kuwa inaendana na mahitaji ya Serikali na soko la ajira. Alisema programu hiyo itaongeza idadi ya wataalamu wenye ujuzi na uelewa wa kina wa usimamizi wa mali za umma, jambo litakalosaidia kuimarisha uwajibikaji, ufanisi na matumizi sahihi ya rasilimali za Serikali. Ziara hiyo ilifadhiliwa na Kuehne Foundation kupitia Mradi wa LEARN, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha elimu ya juu inayozingatia vitendo na kukuza wataalamu mahiri wa ununuzi na usimamizi wa mali nchini.