News-Details

News >Details

MZUMBE NA KÜHNE FOUNDATION WAIBUA WATAALAMU WA AKILI MNEMBA KATIKA USAFIRISHAJI

MZUMBE NA KÜHNE FOUNDATION WAIBUA WATAALAMU WA AKILI MNEMBA KATIKA USAFIRISHAJI

Chuo Kikuu Mzumbe kwa kushirikiana na Taasisi ya Kühne Foundation kimehitimisha rasmi semina ya siku tatu ya mafunzo ya uvumbuzi katika matumizi ya Akili Mnemba (Artificial Intelligence) katika sekta ya usafirishaji na usimamizi wa mizigo, semina iliyohitimishwa tarehe 19 Disemba 2025. Zaidi ya washiriki 40 walihitimu mafunzo hayo na kukabidhiwa vyeti vya ushiriki. Semina hiyo iliyoanyika Ndaki ya Dar es Salaam, iliwakutanisha wadau wa sekta ya usafirishaji, ugavi na manunuzi pamoja na wanafunzi wa shahada zinazohusiana na fani hizo, kwa lengo la kuwajengea uwezo na ujuzi wa kisasa unaoendana na maendeleo ya teknolojia. Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo kwa niaba ya Rasi wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam, Mratibu wa Mafunzo ya Shahada ya Awali wa ndaki hiyo, Dkt. Janeth Swai, aliwataka washiriki kutumia maarifa na ujuzi walioupata kuleta mabadiliko chanya katika maeneo yao ya kazi, ili kuongeza ufanisi katika sekta za usafirishaji, ugavi na manunuzi nchini. Dkt. Swai aliishukuru Taasisi ya Kühne Foundation kwa kufadhili mafunzo hayo pamoja na washiriki wote kwa ushiriki wao wa kina, akisisitiza kuwa mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha wataalamu kukabiliana na changamoto za kisasa kwa kutumia teknolojia ya Akili Mnemba kwa manufaa ya taasisi wanazozihudumia na taifa kwa ujumla. “Ni matarajio yetu kuwa ujuzi mlioupata utawajengea kujiamini zaidi katika utekelezaji wa majukumu yenu na kuchochea maboresho ya utendaji katika maeneo yenu ya kazi,” alisema Dkt. Swai. Kwa upande wake, Mwakilishi wa Taasisi ya Kühne Foundation nchini Tanzania, Bi. Flora Michael, alisema kuwa lengo la Taasisi hiyo kushirikiana na Chuo Kikuu Mzumbe ni kujenga uwezo wa wataalamu wa sekta ya usafirishaji, usimamizi wa mizigo, ugavi na manunuzi, hususan katika matumizi ya teknolojia ya Akili Mnemba katika shughuli za kila siku. Naye mkufunzi wa mafunzo hayo, Dkt. Enock Mwakalila, alisema kuwa katika kipindi cha siku tatu washiriki walipatiwa mada mbalimbali kwa njia ya vitendo, zikiwemo utangulizi wa Akili Mnemba katika sekta ya usafirishaji, matumizi ya teknolojia hiyo katika uboreshaji wa njia za usafiri, ufuatiliaji wa mizigo kwa kutumia mifumo ya kisasa, usimamizi wa ugavi na manunuzi, pamoja na utabiri wa mahitaji na usimamizi wa rasilimali. Aidha, washiriki wa semina hiyo wamekishukuru Chuo Kikuu Mzumbe kwa kuandaa mafunzo hayo, wakieleza kuwa yameongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao na kuboresha utoaji wa huduma. Hata hivyo, wamekiomba chuo hicho kuendelea kuandaa mafunzo zaidi ya aina hiyo kutokana na mahitaji makubwa ya ujuzi wa teknolojia katika mazingira ya kazi ya sasa. Semina hiyo ilifanyika kwa muda wa siku tatu kuanzia tarehe 17 hadi 19 Disemba 2025, ikiandaliwa na Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam na kudhaminiwa na Taasisi ya Kühne Foundation kupitia Mradi wa LEARN.

None