Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Mhe. Gilbert Kalima, leo amefanya ziara rasmi ya kukagua utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi ya Tanga, hatua aliyosema ni ya kihistoria na yenye manufaa makubwa kwa maendeleo ya elimu, uchumi na jamii ya Mkinga na Mkoa wa Tanga kwa ujumla. Ziara hiyo ilihusisha viongozi mbalimbali wa Wilaya akiwemo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga Mhe. Amani J. Kisinya, Katibu Tawala wa Wilaya Mhe. Mwanamwaya Kombo, pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, huku uongozi wa Chuo Kikuu Mzumbe ukiongozwa na Makamu Mkuu wa Chuo Prof. William Mwegoha, akiambatana na sehemu ya Menejimenti na viongozi wa Mradi wa HEET. Awali, Prof. Mwegoha aliwasilisha taarifa ya mradi akieleza kuwa ujenzi wa kampasi hiyo umefikia asilimia 80, hatua inayotoa matumaini makubwa ya kuanza kupokea wanafunzi kuanzia mwaka wa masomo 2026/2027. Prof. Mwegoha amesisitiza kuwa Chuo Kikuu Mzumbe kimejipanga kikamilifu kuhakikisha kampasi ya Tanga inakuwa kituo imara cha elimu ya juu kinachozingatia viwango vya kitaifa na kimataifa, sambamba na mpango mkakati wa chuo wa miaka mitano unaoanza utekelezaji wake Julai 2026. “Kampasi hii ni mtoto wetu. Tumejidhatiti kuisimamia, kuikuza na kuifikisha katika viwango vinavyostahili. Tumeanza maandalizi ya kitaasisi, kitaaluma na miundombinu ili kuhakikisha inakuwa kampasi kamili na shindani,” alisema Prof. Mwegoha. Akizungumza baada ya ukaguzi wa mradi, Mhe. Gilbert Kalima ameipongeza menejimenti ya Chuo Kikuu Mzumbe kwa usimamizi thabiti wa mradi huo, akisema ujenzi unaoendelea unaakisi uadilifu, uwajibikaji na heshima ya taasisi hiyo kongwe. Aidha, amewataka wakandarasi kuhakikisha wanakamilisha kazi kwa wakati kulingana na nyongeza ya muda waliyopewa, akisisitiza kuwa uzembe wowote hautavumiliwa. “Hii ni fursa ya kipekee kwa wananchi wa Mkinga, Gombero na Mkoa wa Tanga. Mradi huu ni chachu ya maendeleo. Ni wajibu wetu wote kushirikiana kuhakikisha fedha za serikali zinaleta tija iliyokusudiwa,” alisema Mhe. Kalima. Mhe. Kalima pia aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha fedha nyingi za utekelezaji wa mradi huo, akibainisha kuwa zaidi ya dola za kimarekani Milioni saba zimeelekezwa katika kampasi hiyo kama sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa HEET. Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Mkinga, Bi. Mwanamwaya Kombo, amesema uwekezaji wa Chuo Kikuu Mzumbe Gombero ni fursa adhimu ya kukuza uchumi wa eneo hilo kupitia ajira, biashara ndogondogo, huduma za malazi na chakula. “Chuo hiki si cha Mzumbe pekee, ni cha wananchi. Wananchi wa Gombero wachangamkie fursa hizi ili kujikwamua kiuchumi,” alisema. Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga, Mhe. Amani J. Kisinya, alisema ujio wa Chuo Kikuu Mzumbe umeiweka Mkinga katika ramani ya kitaifa na kimataifa, akilitaja chuo hicho kuwa ni taasisi yenye hadhi kubwa duniani. Kwa upande mwingine, Mratibu wa Mradi huo Chuo Kikuu Mzumbe ambaye pia ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma, Utafiti na Ushauri, Prof. Hawa Tundui, amesema mradi huo unalenga kuandaa wahitimu wenye ujuzi wa ajira na ujasiriamali, sambamba na kuchochea mabadiliko ya kiuchumi katika jamii inayozunguka kampasi. “Mradi huu haujajikita kwenye majengo pekee, bali unalenga kubadili fikra, maarifa na uwezo wa vijana ili wawe waajiriwa au waajiri,” alisema Prof. Tundui. Ziara ya Mkuu wa Wilaya imeacha taswira chanya ya dhamira ya serikali, Chuo Kikuu Mzumbe na jamii ya Mkinga kushirikiana katika kuujenga na kukamilisha mradi unaotarajiwa kuwa nguzo muhimu ya elimu ya juu, ajira na maendeleo endelevu kwa kizazi cha sasa na kijacho.