Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha, amewakabidhi rasmi wanafunzi ambao ni wanamichezo 80 wa Chuo hicho watakaokiwakilisha Chuo katika Mashindano ya Shirikisho la Vyuo Vikuu Tanzania (TUSA) 2025, yatakayofanyika katika Chuo Kikuu cha Dodoma kuanzia tarehe 15 hadi 23 Desemba 2025. Akizungumza katika hafla ya kuwaaga wanamichezo hao iliyofanyika chuoni hapo, Prof. Mwegoha alisema: "Michezo inaendana moja kwa moja na taswira ya Chuo. Hivyo, zingatieni nidhamu, muwe washindani wa kweli na mhakikishe mnapeperusha vyema bendera ya Chuo mtakapokuwa kwenye Mashindano." Aliongeza pia kuwa wanapaswa kujilinda, kushirikiana vyema, na kuhakikisha wanarejea na vikombe vingi vya ushindi. Kwa upande wake, Mkufunzi wa Michezo wa Chuo Kikuu Mzumbe, Bw. Daniel Kintingu, alisema kuwa Chuo hicho kinatarajia kushiriki mashindano hayo kwenye michezo 15 mbalimbali, ikiwemo: mpira wa miguu, mpira wa kikapu, mpira wa netiboli, mpira wa wavu, handball, woodball, riadha, tenisi, Table Tennis, chess, Mchezo wa maneno (scrabble), pooltable, nage/rede kwa wanawake, pamoja na goal ball. AidhaMkufunzi huyo alianisha kuwa katika kujiweka sawa katika Mashindano hayo Wanamichezo wote watakuwa kwenye kambi iliyopo Shule Ya Sekondari Dr. Samia Iliyopo Jijini Dodoma. Vilevile, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo - Taaluma, Utafiti na Ushauri, Prof. Hawa Tundui aliwaasa wanamichezo kuzidi pia kuweka jitihada za kitaaluma na kuwa na matokeo mazuri kama ambavyo wanatafuta matokeo mazuri ya kimichezo. Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo - Mipango, Fedha na Utawala, Prof. Allen Mushi, aliwakumbusha wanamichezo hao kuwa michezo inahitaji nidhamu ya hali ya juu, hasa wanapokuwa wanaiwakilisha nchi nje ya mipaka ya Tanzania. Alisema: "Mbali na kupeperusha bendera ya Chuo Kikuu Mzumbe, pia mnapeperusha bendera ya nchi yetu, hivyo hakikisheni mnaleta heshima kwa wote." Chuo Kikuu Mzumbe kinazidi kuonyesha dhamira yake ya kukuza michezo na kuimarisha ushirikiano wa kitaaluma na michezo, huku kikiendelea kuiishi kauli mbiu yake ya “Tujifunze Kwa Maendeleo ya Watu”.