Chuo Kikuu Mzumbe kupitia Kitivo cha Sayansi za Jamii kimewezesha wanafunzi wa mwaka wa pili wa Shahada ya Sayansi ya Uchumi (Bachelor of Science in Economics) kushiriki katika ziara ya mafunzo katika Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA). Ziara hiyo ilihusisha wanafunzi kutoka katika programu tatu za shahada ambazo ni Shahada ya Sayansi ya Uchumi – Idadi ya Watu na Maendeleo, Shahada ya Sayansi ya Uchumi – Mipango na Usimamizi wa Miradi, na Shahada ya Sayansi ya Uchumi – Sera na Mipango ya Uchumi. Ziara hiyo, imefanyika tarehe 6 Februari 2025 chini ya mradi wa HEET, ililenga kuwapa wanafunzi uelewa wa kina kuhusu mchango wa bandari katika uchumi wa nchi pamoja na usimamizi wa shughuli mbalimbali zinazofanywa na mamlaka hiyo. Mkurugenzi wa Mipango, Ubora na Vihatarishi wa Mamlaka hiyo, Dkt. Boniphace Nopeji, aliwakaribisha wanafunzi na kuwaeleza kuhusu majukumu ya mamlaka hiyo katika kusimamia na kuboresha huduma za bandari. Alieleza kuwa bandari ni nyenzo muhimu katika kukuza uchumi wa taifa kupitia usafirishaji wa bidhaa ndani na nje ya nchi. Dkt. Nopeji aliwataka wanafunzi kutumia fursa hiyo kuongeza maarifa na kuelewa kwa undani namna sekta ya bandari inavyochangia katika mipango ya maendeleo ya kiuchumi. Aidha, Wanafunzi walinufaika na maelezo ya kina kutoka kwa mtaalamu huyo, jambo lililowasaidia kupata uelewa wa hatua mbalimbali za usimamizi wa bandari na mchango wake katika uchumi wa taifa. Ziara hii imewasaidia wanafunzi kuunganisha nadharia wanayojifunza darasani na matumizi yake katika sekta ya bandari, hivyo kuwaandaa vyema kwa mahitaji ya soko la ajira na mchango wao katika maendeleo ya uchumi wa nchi.