Chuo Kikuu Mzumbe ni miongoni mwa Taasisi za Elimu ya Juu 18 zilizoshiriki katika ufunguzi wa Mashindano ya 12 ya Shirikisho la Vyuo Vikuu Tanzania (TUSA), uliofanyika tarehe 17 Disemba 2025 katika Uwanja wa Michezo wa Ndaki ya Kompyuta na Sayansi Angavu, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM). Akifungua rasmi mashindano hayo, Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu ya Juu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Fatihiya Massawe, aliyemwakilisha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mheshimiwa Profesa Adolf Mkenda, alisema kuwa mashindano ya TUSA ni jukwaa muhimu katika kuimarisha afya za wanafunzi, kuibua na kukuza vipaji vya michezo pamoja na kuimarisha mshikamano na umoja miongoni mwa Taasisi za Elimu ya Juu nchini. Prof. Massawe aliongeza kuwa michezo ni nyenzo muhimu katika kujenga nidhamu, uongozi, maadili mema na ushindani wa haki kwa vijana wanaojiandaa kuwa viongozi wa baadaye wa taifa. Aidha, alibainisha baadhi ya changamoto zinazoikabili TUSA, ikiwemo ushiriki mdogo wa wanachama. Alieleza kuwa kwa mwaka 2025, ni Taasisi 18 pekee kati ya Taasisi 45 wanachama zilizoshiriki mashindano hayo. Kutokana na hali hiyo, Prof. Massawe alizihimiza Taasisi ambazo hazikushiriki kujipanga vyema, kuimarisha maandalizi na kushiriki kikamilifu katika mashindano yajayo ili kuendeleza malengo ya shirikisho na kukuza michezo katika vyuo vikuu nchini. Chuo Kikuu Mzumbe kinashiriki mashindano ya mwaka huu katika jumla ya michezo 15, ikiwemo mpira wa miguu, mpira wa kikapu, netiboli, mpira wa wavu, handball, woodball, riadha, tenisi, tenisi ya meza (table tennis), chess, mchezo wa maneno (scrabble), pool table, nage/rede kwa wanawake pamoja na goal ball. Chuo kimejipanga kushinda, kulingana na historia na rekodi yake nzuri katika mashindano ya kitaifa. Kwa miaka mingi, Chuo Kikuu Mzumbe kimeendelea kujijengea heshima na umaarufu mkubwa katika nyanja za elimu, utafiti, ushauri wa kitaalamu pamoja na michezo. Chuo hicho ni miongoni mwa vyuo vinavyoongoza nchini katika kuandaa wahitimu wenye nidhamu, uwezo wa kiutendaji na ushindani wa kitaifa na kimataifa.