Chuo kikuu Mzumbe, Ndaki ya Dar es Salaam kimeendesha mafunzo maalumu kwa wanafunzi wa Shahada ya kwanza na shahada ya uzamili kuhusu matumizi ya rasilimali za kielektroniki zinazopatikana chuoni hapo. Mafunzo hayo yaliyofanyika Disemba 12, 2025 yamelenga kuwasaidia wanafunzi kupata taarifa sahihi na za kuaminika kwa ajili ya kazi zao za kitaaluma. Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo Mkuu wa Kitengo cha huduma za Maktaba Ndaki ya Dar es Salaam Bw. Elias Ntobi amewataka wanafunzi wote kuzingatia mafunzo hayo kwani itawasaidia katika utekelezaji sahihi wa maandiko yao ya kitaaluma ikiwa ni pamoja na tafiti watakazoziandika ili kuepukana na matumizi yasiofaa ya akili unde katika kazi za kitaaluma. Aidha Bw. Ntobi ameongeza kuwa wanafunzi hao watafundishwa mbinu mbalimbali za kutafuta na kurejesha taarifa (searching and retriving information) na zana mbalimbali za usimamizi rejea (Reference Management Tools), kupitia mfumo wa kisasa wa maktaba kiganjani (Myloft Application). Kwa upande wake Afisa Maktaba Bw. Bernard Msengi amewaongoza washiriki katika namna bora ya kutumia kanzidata na vyanzo mbalimbali vya taarifa ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wanafunzi na walimu. Huku akisisitiza umuhimu wa watumishi wa huduma za maktaba kujifunza mara kwa mara kuhusu matumizi sahihi ya maktaba mtandao. Aidha, mada ya zana za usimamizi rejea iliyowasilishwa na Afisa Maktaba, Bw. Mkomwa Moshi, aliyewaelekeza wanafunzi hao juu ya matumizi sahihi ya zana za kusimamia marejeo kama vile Mendeley na Zotero, kwa lengo la kuwasaidia wanafunzi katika tafiti zao na kuandaa maandiko yao kwa usahihi na kufuata viwango vya kitaaluma. Kwa upande wao wanafunzi walioshiriki mafunzo hayo wamekishukuru Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam kupitia huduma za maktaba kwa kuandaa mafunzo hayo kwani itawawezesha kupata vitabu na Makala mbalimbali ya miaka ya karibuni kwa urahisi na nafuu katika kuandaa kazi zao za kitaaluma. Aidha wameahidi kuwa waaminifu katika kazi zao za kitaaluma kulinda Imani ya chuo chao na sifa bora iliyopo kitaifa na kimataifa.