News-Details

News >Details

MADARASA YA KISASA YA UJIFUNZAJI KIDIGITALI YAZINDULIWA MZUMBE

MADARASA YA KISASA YA UJIFUNZAJI KIDIGITALI YAZINDULIWA MZUMBE

Chuo Kikuu cha Mzumbe kimezindua madarasa mawili ya kisasa ya ujifunzaji kidigitali katika Kampasi Kuu ya Morogoro, hatua inayolenga kuboresha ufundishaji na ujifunzaji kwa kutumia teknolojia ya kisasa na kuimarisha mfumo wa ufundishaji mseto Miundombinu ya kidigitali katika madarasa hayo imewezeshwa na Mradi wa NISHATI, unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya, ambao unalenga kujenga uwezo, kukuza ubunifu na kuimarisha ukuaji wa vyuo vikuu sita barani Afrika, pamoja na Chuo cha Cadiz kutoka Spain na Chuo Kikuu Sapienza Rome, Italia. Uzinduzi huo umefanyika leo tarehe 9 Januari 2026 na kuambatana na mafunzo ya awali ya matumizi ya vifaa chini ya kaulimbiu “Kuimarisha Ufundishaji na Usimamizi wa Madarasa Kupitia Teknolojia ya Kisasa.” Akizungumza wakati wa uzinduzi, Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. William Mwegoha amesema “madarasa hayo yataongeza ubora wa ufundishaji na ujifunzaji, kuwajengea wahadhiri uwezo wa kitaaluma na kuwapa wanafunzi uzoefu wa kisasa wa teknolojia”. Amewahimiza wahadhiri kutumia kikamilifu madarasa hayo na kuhakikisha vifaa vinatunzwa ipasavyo. Kwa upande wake Naibu Makamu Mkuu Taaluma, Utafiti na Ushauri, Prof. Hawa Tundui, amesema uzinduzi huo ni mwanzo mzuri wa kuimarisha mfumo wa ufundishaji mchanganyiko na kusisitiza umuhimu wa kuendelea kuboresha miundombinu ya kiteknolojia. Awali Amidi wa Shule ya Utawala wa Umma na Menejimenti ambaye pia ni mratibu wa mradi wa NISHATI, Prof. Idda Lytonga Swai, amesema madarasa hayo yatatumika kama vituo vya mafunzo kwa wahadhiri na wanafunzi, sambamba na kaulimbiu ya chuo “Tujifunze kwa Maendeleo ya Watu.” Naye Mwakilishi wa wanafunzi, Bw. Odax Rukiza, alisema uwekezaji huo utarahisisha ujifunzaji, kuongeza uzoefu wa kisasa na kuvutia wanafunzi wengi zaidi. Akitoa neno la shukrani, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Mipango, Fedha na Utawala, Prof. Allen Mushi, aliipongeza timu iliyoratibu tukio hilo na kueleza kuwa chuo kinaendelea kuboresha madarasa zaidi kulingana na mahitaji ya elimu ya kisasa. Uzinduzi huu unaonesha dhamira ya Chuo ili kuimarisha teknolojia ya elimu na kuchochea maendeleo endelevu kupitia matumizi ya teknolojia.

None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None