News-Details

News >Details

MZUMBE NA ALAT WASHIRIKIANA KUIMARISHA UONGOZI NA MAENDELEO YA KATA YA MZUMBE

MZUMBE NA ALAT WASHIRIKIANA KUIMARISHA UONGOZI NA MAENDELEO YA KATA YA MZUMBE

Chuo Kikuu Mzumbe kwa kushirikiana na Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) wameendesha mafunzo maalumu ya uongozi na utawala kwa viongozi wa Serikali za Vijiji na Vitongoji wa Kata ya Mzumbe, wilayani Mvomero, yakilenga kujenga uwezo wa viongozi na kuimarisha utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika ngazi ya jamii. Mafunzo hayo yamefanyika tarehe 09 Januari 2026 katika Ukumbi wa Luthuli – Kampasi Kuu ya Chuo Kikuu Mzumbe, Morogoro. Mafunzo hayo yalijikita katika kujadili masuala makuu ya uongozi, maendeleo pamoja na ushiriki wa wananchi katika shughuli za maendeleo, yakitafsiriwa na washiriki kama mwanzo mzuri wa mwaka kwa viongozi wa Serikali za Vijiji na Vitongoji wa Kata ya Mzumbe. Akifungua mafunzo hayo, Amidi wa Shule ya Utawala wa Umma na Menejimenti (SoPAM) ya Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. Idda Lyatonga, alieleza kuwa licha ya viongozi wengi kuwa na uzoefu mkubwa wa kiutendaji, mafunzo hayo ni jukwaa muhimu la kukumbushana, kubadilishana uzoefu na kuimarisha mbinu bora za uongozi kwa manufaa ya maendeleo ya Kata ya Mzumbe kwa ujumla. Aidha, aliipongeza Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu Mzumbe katika kuandaa mafunzo hayo, akieleza kuwa ushirikiano huo ni kielelezo cha dhamira ya pamoja ya kuimarisha utawala bora na maendeleo ya wananchi. Prof. Lyatonga alisisitiza kuwa maendeleo ya kweli ya Kata ya Mzumbe yatapatikana pale kila kijiji kitakapotekeleza majukumu yake kwa ufanisi, akibainisha kuwa mafanikio ya kijiji kimoja ni mafanikio ya kata nzima. “Mnatoka vijiji na vitongoji tofauti, lakini mkifanikiwa kila mmoja katika eneo lake, mnafanikiwa kwa pamoja kama Kata ya Mzumbe,” alisema Prof. Lyatonga. Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mzumbe, Mhe. Ferdinand Stanslaus, aliipongeza Chuo Kikuu Mzumbe kwa kuendelea kuwa mshirika wa karibu wa viongozi wa kata, vijiji na vitongoji, katika masuala ya elimu, uongozi na maendeleo ya jamii. “Chuo Kikuu Mzumbe kimekuwa karibu sana na wananchi wake. Kimekuwa kikitushirikisha katika shughuli za elimu na maendeleo, na sisi kama viongozi wa kata, vijiji na vitongoji tuko tayari kushirikiana nacho wakati wote,” alisema Mhe. Stanslaus. Kwa ujumla, washiriki wa mafunzo hayo walipongeza juhudi za Chuo Kikuu Mzumbe na ALAT kwa kuandaa mafunzo yenye tija, wakieleza kuwa yamewapa uelewa mpana na motisha mpya ya kuimarisha uongozi, ushirikishwaji wa wananchi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika vijiji na vitongoji vya Kata ya Mzumbe.

None
None
None
None
None
None
None
None