News-Details

News >Details

WANAFUNZI NDAKI YA MBEYA WAPATIWA MAFUNZO YA STADI ZA MSINGI (SOFT SKILLS)

WANAFUNZI NDAKI YA MBEYA WAPATIWA MAFUNZO YA STADI ZA MSINGI (SOFT SKILLS)

Chuo Kikuu Mzumbe, kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), kimendeleza mpango maalumu wa mafunzo ya stadi za msingi (soft skills) kwa wanafunzi wa Ndaki ya Mbeya. Mafunzo haya yanahusisha mawasiliano bora, matumizi ya TEHAMA, mwongozo wa kazi na ushauri, ubunifu na ujuzi wa utatuzi wa changamoto ili kuwaandaa vyema kwa soko la ajira na fursa za kujiajiri. Akifungua mafunzo hayo tarehe 8 Januari 2026 katika ukumbi wa Nkurumah Ndaki ya Mbeya, Naibu Rasi wa Ndaki hiyo, Prof. Charles Tundui, alisema soko la ajira limebadilika na linahitaji wataalamu wenye ujuzi mtambuka. “Waajiri wa sasa wanapendelea watu wenye uwezo wa kuwasiliana kwa ufanisi, kushirikiana na wengine, na kuchangia maendeleo ya kijamii na kitaaluma. Stadi hizi ni muhimu kwa wanafunzi kujenga mustakabali wao,” alisema Prof. Tundui. Aliongeza kuwa wanafunzi hawapaswi kutegemea maarifa ya taaluma yao pekee, bali wanapaswa kujifunza na kutumia ujuzi wa ziada ili kufanikisha malengo yao. “Lengo ni kuhakikisha wahitimu wa Mzumbe wanajivunia maarifa yanayowawezesha kushindana katika mazingira yoyote ya kazi,” alisisitiza Prof. Tundui. Kwa upande wake, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Mzumbe ambaye pia ni Mratibu wa Kituo cha Umahiri katiks Ufundishaji na Ujifunzaji Kiubunifu upande wa HEET, Dkt. Perpetua Kalimasi alizungumza kuhusu umuhimu wa mafunzo hayo na kuainisha kuwa mafunzo hayo yanalenga kutoa ujuzi na stadi muhimu kwa wanafunzi zitakazowasaidia katika taaluma na maisha nje ya taaluma. Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Mzumbe na Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Dkt. Mustapha Juakali alieleza umuhimu wa Mwongozo wa Taaluma na Ushauri Nasaha (Career Guidance and Counseling). Alisema huduma hii huwasaidia wanafunzi kutambua vipaji vyao, kuongeza maarifa kwenye taaluma zao, uelewa wa mahitaji ya soko la ajira pamoja na kufanikisha malengo yao kwa kuzingatia uwezo na matarajio yao binafsi. Naye, Mhadhiri Mwandamizi ambaye pia ni Mudiri wa Idara ya Elimu na Ufundishaji Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Haruni Machumu, akizungumzia mada ya maarifa yenye ufanisi katika mawasiliano alieleza kwamba wanafunzi wanapaswa kuwa na ujuzi wa kuwasilisha hoja na kujieleza kwa ufanisi na kusikiliza kwa makini ili kuwa bora kwenye eneo la mawasiliano . “Ujuzi huu utawasaidia kuwa viongozi bora, kushirikiana vyema na wengine, na kufanikisha malengo yao katika mazingira ya kazi,” alisema Dkt. Machumu. Aidha, Mkurugenzi wa Huduma za Maktaba wa Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Kardo Mwilongo, alisisitiza umuhimu wa elimu ya kidijitali. Alisema, “Wanafunzi wanapaswa kujifunza jinsi ya kutumia teknolojia za kisasa kama kompyuta na mitandao kwa njia bora na salama ili kuongeza tija na ufanisi katika kazi zao.” Katika mafunzo hayo, wanafunzi walipata wasaa wa kuuliza maswali na kutoa maoni juu ya mafunzo hayo, pia wanafunzi walionesha kufurahia mafunzo hayo na uhitaji wa kupata mafunzo ya namna hiyo mara kwa mara ili kuongeza maarifa, uelewa na kujenga uwezo kitaaluma na binafsi. Akihitimisha mafunzo hayo, Afisa Rasilimali Watu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Mbeya, Bw. Lusajo Ngabo aliwaasa wanafunzi kuyafanyia kazi mafunzo ili yawafungue fikra zao zaidi na kuwapa maarifa muhimu yatakayowasaidia, si tu chuoni, bali pia katika maisha yao ya baadaye.

None
None
None
None
None
None
None
None
None
None