News-Details

News >Details

CHUO KIKUU MZUMBE KUIMARISHA MBINU BORA ZA UFUNDISHAJI

CHUO KIKUU MZUMBE KUIMARISHA MBINU BORA ZA UFUNDISHAJI

Chuo Kikuu Mzumbe kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) kimeendesha mafunzo maalumu ya matumizi ya mfumo wa ujifunzaji kwa njia ya kielektroniki (e-Learning) kwa Wanataluma wa Ndaki ya Mbeya, lengo likiwa ni kuboresha mbinu za ufundishaji kwa njia ya mtandao na kuchochea uandaaji wa maudhui shirikishi mtandaoni, mwishoni mwa wiki. Katika mafunzo hayo, Wanataaluma walijifunza namna ya kuandaa kozi/programu, jinsi ya kuwezesha wanafunzi kujiunga wenyewe (self-enrollment), kuunda makundi ya wanafunzi darasani, kupanga na kuingiza alama (grading), pamoja na maandalizi na uendeshaji wa madarasa kwa kutumia jukwaa la Zoom kwenye mfumo wa ujifunzaji kieletroniki (eLearning). Mhadhiri Mwandamizi na Mwezeshaji wa mafunzo hayo Dkt. Mustapha Almasi alisisitiza kuwa matumizi ya teknolojia katika ufundishaji ni njia bora ya kuwafikia wanafunzi kwa urahisi na ufanisi, haswa katika ulimwengu wa sasa wa kidigitali. Naye, Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA na Mratibu wa HEET upande wa kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Kidigitali, Dkt. Mohamed Ghasia alieleza kuwa ujuzi wa mfumo wa eLearning kwa Mwanataaluma wa Chuo Kikuu Mzumbe hauepukiki. Mzumbe imejipanga kuendelea kujenga uwezo kwa Wanataaluma ili kuboresha ufundishaji na ujifunzaji. Aidha, Mhadhiri Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Mbeya, Dkt. Adrian Barongo alishukuru wawezeshaji wa mafunzo hayo kwa maarifa yaliyotolewa wakati wa mafunzo na kusisitiza kuwa mafunzo ya namna hiyo yaendelee kufanyika mara kwa mara kwa watumishi wa Chuo Kikuu Mzumbe. Mafunzo hayo yalisimamiwa na Wataalamu wa Mifumo ya Ujifunzaji Kieletroniki kutoka Kitengo cha TEHAMA Chuo Kikuu Mzumbe, Bi. Halima Rajabu na Bw. Abuu Mshamu waliowaongoza washiriki kutumia mfumo wa eLearning kwa ufanisi kupitia mazoezi kwa vitendo. Kupitia mafunzo hayo muhimu, Chuo Kikuu Mzumbe kinaamini kupitia mafunzo hayo yatachochea ubora wa elimu katika kuongeza ushiriki wa mwanafunzi, kuboresha uwezo wa kukumbuka ulichosoma, kusaidia kujifunza kwa vitendo, kutoa mrejesho wa haraka pamoja na kukuza fikra makini.

None
None
None
None
None
None
None