Wanafunzi wa Shahada ya Sheria kutoka Chuo Kikuu Mzumbe wameibuka kidedea baada ya kushiriki na kufanya vyema katika mashindano ya Mahakama Igizi yaliyoshirikisha vyuo vikuu vinavyotoa shahada ya sheria mkoani Morogoro, yaliyofanyika Chuo Kikuu Kishiriki cha Jordan (JUCO), Morogoro, Januari 2026. Mashindano hayo yaliwakutanisha wanafunzi wa sheria kutoka Chuo Kikuu Mzumbe, Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Morogoro na Chuo Kikuu Kishiriki cha Jordan yakitoa jukwaa la kitaaluma kwa wanafunzi kuonesha uwezo wao wa kuendesha mashauri ya kisheria, kuwasilisha hoja kwa kuzingatia taratibu za mahakama na kutetea masuala ya haki za binadamu kwa misingi ya sheria. Akifafanua kuhusu maandalizi na muktadha wa mashindano hayo, Mratibu wa Mahakama Igizi na Huduma za Msaada wa Kisheria wa Chuo Kikuu Mzumbe, Wakili Bernadetha Iteba, alisema kuwa shauri lililotumika katika mashindano hayo lilihitaji wanafunzi kuchambua kwa kina masuala ya haki za binadamu na kuyaweka katika mfumo wa hoja za kisheria zinazokubalika mahakamani. Katika mashindano hayo, timu ya Chuo Kikuu Mzumbe iliyoundwa na Godfrey Gama, Tabitha Ndabila, Reuben Ifinyongolo na Charles Mjanasa, ilisimama kama waleta maombi, huku timu ya Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Morogoro ikijibu hoja hizo kama wajibu maombi, hali iliyotoa ushindani wa hoja uliojaa mbinu na tafsiri tofauti za sheria. Uendeshaji wa mashindano hayo ulisimamiwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mheshimiwa Barabara, huku mgeni rasmi akiwa Hakimu Mkazi Mkuu, Mheshimiwa Lameck Mwamkoa, wote kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, waliotoa tathmini ya kitaaluma kuhusu ubora wa hoja, lugha ya kisheria na utii wa taratibu za mahakama. Baada ya tathmini ya kina, timu ya Chuo Kikuu Mzumbe ilipata alama 83 kati ya 100 dhidi ya timu ya Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro, ushindi uliotokana na mpangilio mzuri wa hoja, ufasaha wa uwasilishaji na matumizi sahihi ya misingi ya kisheria katika kushughulikia shauri husika. Mashindano hayo yameendelea kuwa sehemu muhimu ya kukuza uzoefu wa vitendo kwa wanafunzi wa sheria, huku yakitoa fursa ya tathmini ya kitaaluma kutoka kwa wataalamu wa mahakama na kuimarisha ushindani wa kielimu kati ya vyuo vikuu vya kanda ya Morogoro.