Wanafunzi wa Shahada ya Awali ya Menejimenti ya Mazingira kutoka Taasisi ya Taaluma za Maendeleo, Chuo Kikuu Mzumbe, kwa kushirikiana na wanataaluma wao, wametembelea Kituo cha MEHAYO kinachohudumia na kuwaelimisha watoto na vijana wenye mahitaji maalumu kilichopo Mazimbu, mkoani Morogoro, mwishoni mwa wiki. Ziara hiyo imelenga kutoa msaada wa kijamii pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi ya elimu ya juu na jamii inayozunguka, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa dhima ya chuo katika kuchangia maendeleo ya jamii. Awali akitoa neno la ukaribisho, Katibu wa Kituo cha MEHAYO, Bw. Elia Msigara, ameelezea historia ya kuanzishwa kwa kituo hicho, mafanikio yaliyopatikana pamoja na mahitaji na changamoto zinazokikabili kwa sasa. Alieleza kuwa MEHAYO ni kifupi cha MEntally HAndicapped YOuth, shirika la hisani lisilo la kiserikali la Kitanzania lililoanzishwa mwaka 1995 na Bi. Linda Ngido, aliyekuwa mwalimu. Alifafanua kuwa mwanzilishi huyo ni mwanamke shupavu na mwenye msukumo mkubwa ambaye ametoa maisha yake yote kutetea na kukuza haki za watoto na vijana wenye mahitaji maalumu, hususani katika Mkoa wa Morogoro. Katika ziara hiyo, wanafunzi hao walitoa msaada wa mahitaji mbalimbali kwa watoto wanaolelewa katika kituo hicho ikiwa ni pamoja na vyakula, vifaa na vifaa vya usafi, ikiwa ni sehemu ya mchango wao katika kusaidia jamii inayowazunguka na kuonesha moyo wa huruma, upendo na uwajibikaji kwa jamii. Aidha, wanafunzi walishiriki pia katika shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kufua nguo na kufanya usafi katika maeneo tofauti ya kituo hicho, hatua iliyolenga kuimarisha mshikamano baina yao na watoto pamoja na kuwajengea watoto hao hali ya kujiamini na kuthaminiwa. Kwa upande mwingine, ziara hiyo ilishuhudia ushiriki wa baadhi ya wanafunzi wa Shahada ya Kwanza ya Sayansi ya Agronomia kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, ambao waliungana na wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe katika kutoa msaada huo wa pamoja. Ushirikiano huo umeonesha mshikamano na ushirikiano baina ya taasisi za elimu ya juu katika kuchangia maendeleo ya jamii na kuwahudumia makundi yenye mahitaji maalumu. Akitoa shukurani kwa niaba ya watoto wanaoishi katika kituo hicho, Bi.Miriam Bosco, alisema kuwa msaada uliotolewa umeleta faraja kubwa kwao na kuwafanya wajisikie kuthaminiwa na kupendwa na jamii. Aliongeza kuwa msaada huo ni ishara ya upendo wa dhati na moyo wa kujali watu wenye mahitaji maalumu, na kushukuru Chuo Kikuu Mzumbe pamoja na wadau wengine walioshiriki katika ziara hiyo, na kuwasihi waendelee kushirikiana na kituo hicho.