News-Details

News >Details

KIKAO KAZI CHA WARATIBU WA HEET NCHINI CHAFANYIKA KUTATHMINI UTEKELEZAJI WA MRADI

KIKAO KAZI CHA WARATIBU WA HEET NCHINI CHAFANYIKA KUTATHMINI UTEKELEZAJI WA MRADI

Waratibu wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) kutoka Chuo Kikuu Mzumbe wameshiriki katika Kikao Kazi cha siku nne (4) cha Waratibu wa Mradi wa HEET nchini, kilichoandaliwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kwa lengo la kujadili na kutathmini mwenendo wa utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati unaolenga kuboresha na kuimarisha elimu ya juu nchini Tanzania Akifungua kikao hicho leo Januari 13, 2026, katika ukumbi wa Eden Highlands Hotel, Jijini Mbeya, Mgeni Rasmi ambaye pia ni Makamu Mkuu wa Chuo cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), Prof. Aloys N. Mvuma, aliwahimiza washiriki kuendelea kuzingatia viwango vya juu vya weledi, uwajibikaji na ufanisi katika utekelezaji wa shughuli za mradi, pia akielezea kuwa kikao hicho fursa muhimu ya kubadilishana uzoefu, kujifunza kutoka kwa taasisi nyingine na kuongeza mwonekano wa taasisi husika katika utekelezaji wa miradi ya kitaifa. “Ninawasihi waratibu wote kuhakikisha mnafanya kazi kwa weledi na nidhamu ya hali ya juu, kwani mafanikio ya Mradi wa HEET yanategemea kwa kiasi kikubwa uwajibikaji na ushirikiano wenu,” alisema Prof. Mvuma. Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa HEET Kitaifa, Dkt. Kennedy Hosea, aliwasilisha taarifa ya hali ya utekelezaji wa mradi kitaifa, ambapo alieleza kuwa utekelezaji unaendelea vizuri kulingana na viashiria na malengo yaliyowekwa. Dkt. Hosea aliwapongeza waratibu wa mradi pamoja na Kamati ya Utekelezaji wa Mradi kwa kuonesha kiwango cha juu cha weledi, uwajibikaji na mshikamano, hali iliyochangia kwa kiasi kikubwa mafanikio yaliyofikiwa hadi sasa. Katika siku ya kwanza ya kikao hicho, miongoni mwa waliowasilisha mada alikuwa Naibu Mratibu wa Mradi wa HEET wa Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Lihoya Chamwali, ambaye aliwasilisha taarifa ya maendeleo ya utekelezaji wa mradi katika chuo Kikuu Mzumbe. Katika wasilisho lake, Dkt. Chamwali alieleza masuala mbalimbali ikiwemo: Hali ya utekelezaji wa mradi katika maeneo yote ya vipaumbele ya mradi, Mipango ya kimkakati kuelekea kukamilika kwa utekelezaji wa mradi, Mikakati ya kuhakikisha uendelevu wa matokeo ya mradi baada ya kukamilika kwake, Utekelezaji wa maelekezo na mapendekezo ya Ujumbe wa Usaidizi wa Utekelezaji wa Benki ya Dunia uliofanyika kuanzia Novemba 17 hadi 21, 2025. Aidha, Dkt. Lihoya alihitimisha kwakudadavua kiundani Shughuli zilizopangwa kutekelezwa katika kipindi cha miezi sita (6) iliyobaki ya mradi; pamoja na Changamoto kuu zilizojitokeza wakati wa utekelezaji, hatua zilizochukuliwa kuzitatua na mafunzo muhimu yaliyopatikana kwa ajili ya kuboresha utekelezaji wa miradi na programu za baadaye katika sekta ya elimu ya juu. Kikao kazi hicho kinatarajiwa kuendelea hadi Januari 16, 2026, ambapo washiriki kutoka vyuo vikuu na taasisi mbalimbali nchini wataendelea kujadili masuala ya utekelezaji, ufuatiliaji na uendelevu wa Mradi wa HEET.

None
None
None
None
None
None
None
None
None