Chuo Kikuu Mzumbe kupitia Idara ya Usimamizi wa Mifumo ya Afya iliyopo chini ya Skuli ya Utawala wa Umma na Menejimenti kimeandaa kongamano la mwisho wa muhula (End-of-Semester Student Forum) kwa ajili ya wanafunzi wa idara hiyo. Kongamano hilo lililenga kuwaunganisha wanafunzi na kuwaelimisha kuhusu masuala mbalimbali ya kitaaluma na taaluma zao kwa ujumla. Mgeni rasmi wa kongamano ambaye pia ni Amidi wa Skuli ya Utawala wa Umma na Menejimenti, Dkt. Idda Lyatonga ambaye alitoa pongezi kwa Idara ya Usimamizi wa Mifumo ya Afya kwa juhudi zake katika kuwaunganisha wanafunzi na kuwajengea uelewa mpana wa taaluma yao. Aidha, alisisitiza kuwa idara hiyo inaendelea kufanya vizuri katika taaluma, huku ufaulu wa wanafunzi wake ukiwa wa kuridhisha. Katika kongamano hilo, mada mbalimbali ziliwasilishwa na wataalamu kutoka Chuo Kikuu Mzumbe. Mhadhiri wa Chuo, Bw. Mzakiru Twalibu, alitoa mada kuhusu Kanuni na Sera za Wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe, akiwapa wanafunzi mwongozo wa kufuata ili kuhakikisha wanadumu katika misingi ya kitaaluma na maadili ya chuo. Naye, Dkt. Mackfallen Anasel alitoa muhtasari wa historia, hali ya sasa na mwelekeo wa baadaye wa Idara ya Usimamizi wa Mifumo ya Afya, akiwahamasisha wanafunzi kuendelea kuchangamkia fursa zinazotolewa na idara hiyo. Dkt. Godfrey Kacholi, Mratibu wa Idara ya Usimamizi wa Mifumo ya Afya, alitoa mada kuhusu utaalamu na maadili kwa wanafunzi wa idara hiyo, akisisitiza umuhimu wa kuwa na maadili mema katika utendaji kazi wa taaluma zao. Baadhi ya wanafunzi wa shahada za uzamili waliotoa mada ni pamoja na Amos Jeremiah, Festus Tandoo na Geofrey Kombo, ambao walielezea kwa kina kuhusu mtazamo wa waajiri (The Employer’s Perspective), matarajio yao kazini, uzoefu wa maisha chuoni na mipango ya maendeleo kwa taaluma zao katika Usimamizi wa Mifumo ya Afya na Ufuatiliaji na Tathmini (HSM & M&E). Kongamano hilo limepongezwa kwa kuwa jukwaa muhimu la wanafunzi kubadilishana mawazo, kupata mwongozo wa kitaaluma na kujiandaa kwa maisha ya kazi baada ya chuo. Idara ya Usimamizi wa Mifumo ya Afya inaendelea na dhamira yake ya kutoa elimu bora.