News-Details

News >Details

WAJUMBE WA DAWATI LA JINSIA MZUMBE WAJENGEWA UWEZO WA KUPAMBANA NA UKATILI WA KIJINSIA

WAJUMBE WA DAWATI LA JINSIA MZUMBE WAJENGEWA UWEZO WA KUPAMBANA NA UKATILI WA KIJINSIA

Chuo Kikuu Mzumbe kimeendesha mafunzo maalumu kwa Wajumbe wa Baraza la Dawati la Jinsia, hatua inayolenga kuongeza uelewa na uwezo wa dawati hilo katika kushughulikia ukatili wa kijinsia na aina nyingine za ukatili zinazojitokeza ndani na nje ya chuo.Mafunzo hayo, yaliyofanyika tarehe 19 Januari, 2026, Kampasi Kuu Morogoro, yalifunguliwa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Mipango, Fedha na Utawala, Profesa Allen Mushi. Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo Profesa Allen Mushi alisema kuwa Mafunzo hayo ni fursa muhimu ya kuimarisha uelewa wa wajumbe juu ya ukatili wa kijinsia, na kuongeza uwezo wao wa kutambua viashiria vya ukatili na matukio yanapojitokeza. “Tunataka wajumbe wa Dawati la Jinsia waweze kushughulikia malalamiko kwa weledi, kuheshimu faragha ya wahanga, na kuhakikisha usalama wao wakati wote. Kwa kutumia mbinu sahihi na teknolojia, tutarahisisha utoaji wa taarifa na kuunda mazingira salama kwa wote,” alisema Profesa Mushi. Mafunzo hayo yamewalenga wajumbe kuelewa aina mbalimbali za ukatili, hususani ukatili wa kijinsia, kimwili, kisaikolojia, kiuchumi na kingono, na kujenga uwezo wa kushughulikia malalamiko kwa kuzingatia maadili, utu, faragha na usalama wa wahanga. Wajumbe pia walipatiwa mwongozo wa jinsi ya kushughulikia rufaa za wahanga na kuunganishwa na huduma stahiki, zikiwemo afya, kisheria, kisaikolojia na ustawi wa jamii. Kwa upande wake, Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Afisa Maendeleo ya Jamii mwandamizi kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Bw. Emmanuel Maketa, alifundisha mbinu bora za uendeshaji wa Dawati la Jinsia, ikiwemo namna ya kujaza daftari la kusajili vitendo vya ukatili wa kijinsia na kuhakikisha taarifa zinakusanywa kwa ufasaha na usiri. Aliwahimiza kutumia mbinu hizo kwa weledi ili kuongeza ufanisi wa dawati na kuimarisha imani ya waathirika. Naye Mshauri wa Wanafunzi kutoka Kurugenzi ya Huduma za Wanafunzi ya Chuo Kikuu Mzumbe, Bw. Alphonce Kauky, alieleza kuwa Dawati la Jinsia ni nyenzo muhimu ya kulinda ustawi wa wanafunzi na wafanyakazi wa chuo. Aliongeza kuwa licha ya jitihada zinazofanywa, changamoto kama hofu ya wahanga kutoa taarifa na upungufu wa rasilimali bado zinahitaji uelewa zaidi na mbinu bora. Mafunzo yalijikita katika kutoa elimu na uhamasishaji kama njia ya kuzuia ukatili, kwa kuandaa na kutekeleza programu kwa wanafunzi, wafanyakazi na jamii inayozunguka Chuo. Wajumbe pia walihimizwa kuendeleza mtazamo chanya wa usawa wa kijinsia na heshima kwa makundi yote, kama mkakati wa muda mrefu wa kuimarisha mazingira salama ya kujifunzia na kufanya kazi.

None
None
None
None
None
None
None
None
None