Kamati ya Uendeshaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) ya Chuo Kikuu Mzumbe imemhimiza mkandarasi wa ujenzi Kampasi ya Tanga kuhakikisha anakamilisha kazi kwa wakati, kwa ufanisi na kwa kuzingatia viwango vya juu vya ubora, ili mradi huo uweze kuwa na tija iliyokusudiwa kwa jamii na taifa kwa ujumla. Kauli hiyo ilitolewa tarehe 19 Januari 2026 wakati wa ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa Kampasi ya Tanga, iliyoongozwa na Naibu Mratibu wa Mradi wa HEET Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Lihoya Chamwali. Alisema kuwa pamoja na kuridhishwa na kasi ya ujenzi inayoonekana, ni muhimu mkandarasi akaendelea kuongeza juhudi ili kuhakikisha mradi unakamilika ndani ya muda uliopangwa. Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Dkt. Chamwali alisisitiza kuwa utekelezaji wa mradi huo una umuhimu mkubwa katika kufanikisha malengo ya HEET ya kuleta mageuzi ya kiuchumi kupitia elimu ya juu. “Mradi huu ni wa kimkakati kwa Chuo Kikuu Mzumbe na kwa maendeleo ya Mkoa wa Tanga. Tunamhimiza mkandarasi kuendelea kufanya kazi kwa bidii, kuzingatia ratiba na kuhakikisha kuwepo na ubora wa juu, ili Kampasi ya Tanga ikamilike kwa wakati na ianze kutoa huduma zilizokusudiwa,” alisema Dkt. Chamwali. Kwa upande wake, Msimamizi wa Ujenzi wa Kampasi ya Tanga, Bw. Prosper Leonard, alisema kuwa ukaguzi unaoendelea kufanywa na kamati unalenga kuhakikisha kuwa kila hatua ya ujenzi inatekelezwa kwa ufanisi, kwa kuzingatia ubora wa kazi na matumizi ya vifaa vinavyokidhi viwango vilivyowekwa. “Tumesisitiza kwa mkandarasi umuhimu wa kuoanisha kasi ya ujenzi na ubora wa kazi, ili Kampasi ya Tanga iweze kukidhi mahitaji ya elimu ya juu na miundombinu ya kisasa,” alisema Bw. Leonard. Ujenzi wa Kampasi ya Tanga ya Chuo Kikuu Mzumbe unategemewa kukamilika mwezi Machi 2026, na unalenga kuchangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa eneo hilo kwa kuongeza fursa za ajira kwa wakazi, kuimarisha upatikanaji wa elimu ya juu, na kutoa programu mbalimbali za elimu zitakazosaidia kukuza rasilimali watu na maendeleo endelevu ya taifa.