Wajumbe wa Kamati ya Uendeshaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) wa Chuo Kikuu Mzumbe, tarehe 20 Januari 2026, walifanya ziara ya kikazi katika Kampasi Kuu ya Morogoro kwa lengo la kukagua na kutathmini maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi inayotekelezwa chini ya Mradi wa HEET. Ziara hiyo ililenga kujiridhisha na hatua za utekelezaji, ubora wa kazi pamoja na ulinganifu wa miradi hiyo na malengo ya mradi. Ziara hiyo iliongozwa na Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. Hawa Tundui, na iliwahusisha Waratibu wa Mradi wa HEET pamoja na wajumbe wa Menejimenti ya Chuo Kikuu. Kwa pamoja, walipata maelezo ya kina kuhusu utekelezaji wa miradi hiyo na kutoa ushauri wa kitaalamu juu ya maeneo yanayohitaji kuimarishwa ili kuhakikisha thamani ya uwekezaji wa Mradi wa HEET inalindwa na kuendelezwa. Katika ziara hiyo, Kamati ilikagua maendeleo ya ujenzi wa Jengo la Taaluma, Jengo la TEHAMA, mabwawa ya majitaka pamoja na tenki la kuhifadhi maji safi. Aidha, wajumbe walijionea namna miradi hiyo inavyotekelezwa kwa kuzingatia mahitaji ya kitaaluma, kiutawala na huduma muhimu za Chuo Kikuu. Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Prof. Tundui alisisitiza kuwa utekelezaji wa miradi ya HEET haupaswi kuzingatia tu kukamilika kwa majengo, bali pia ubora wake wa muda mrefu na mchango wake katika kuboresha mazingira ya kufundishia, kujifunzia na kufanya utafiti. Alieleza kuwa Chuo Kikuu kitaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi hiyo ili kuhakikisha inakidhi matarajio ya mradi na wadau wake. “Ukaguzi huu ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha kuwa miradi yote ya HEET inatekelezwa kwa ufanisi na kwa kuzingatia vigezo vya kitaalamu vilivyowekwa,” alisema Prof. Tundui. Awali, Mshauri Elekezi kutoka Kampuni ya Y&P Architect, Mhandisi Fadhili Msemo, alieleza kuwa hadi wakati wa ukaguzi huo, ujenzi wa Jengo la Taaluma ulikuwa umefikia asilimia 73, huku Jengo la TEHAMA likiwa limefikia asilimia 75. Hivyo, utekelezaji wa jumla wa majengo ya kitaaluma ulikuwa umefikia asilimia 75. Aliongeza kuwa mabwawa ya majitaka yalikuwa yamefikia asilimia 68, wakati tenki la kuhifadhi maji safi pamoja na eneo la kutupa taka ngumu vilikuwa vimefikia wastani wa asilimia 75. Kwa ujumla, utekelezaji wa miundombinu ya huduma ulikuwa umefikia asilimia 65. Kamati ilibainisha kuwa utekelezaji wa miradi hiyo ya ujenzi unaweka msingi imara wa maendeleo ya baadaye ya Chuo Kikuu Mzumbe, kwani miundombinu inayojengwa itasaidia upanuzi wa programu za elimu, utafiti na ubunifu, sambamba na mahitaji yanayobadilika ya jamii na uchumi wa taifa.