Chuo Kikuu Mzumbe kimeendesha Mafunzo ya Mipango ya Uendelezaji wa Uongozi (Succession Plan) kwa Wajumbe wa Menejimenti, kwa lengo la kujengea uwezo viongozi kuhusu urithishanaji wa madaraka na uendelevu wa uongozi ndani ya taasisi. Mafunzo hayo yamefanyika tarehe 26 Januari 2026 katika Kampasi Kuu ya Chuo Kikuu Mzumbe, Morogoro, yakitolewa na Dkt. Mike Salu kutoka ‘Evolve Board Consulting’. Akifungua mafunzo hayo Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha chuo kinaweka misingi imara ya kuandaa viongozi wa sasa na wa baadae, ili kudumisha ufanisi, uwajibikaji na uthabiti wa uongozi katika utekelezaji wa majukumu ya chuo. “Mpango wa uendelezaji wa uongozi ni nyenzo muhimu katika kuimarisha utawala bora hivyo viongozi wanapaswa kutambua na kutekeleza kwa vitendo. Alisisitiza Prof. Mwegoha. Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. Allen Mushi, amesema kuwa Mpango ya Uendelezaji wa Uongozi (Succession Plan) ni sehemu muhimu ya usimamizi wa rasilimali watu na maendeleo ya taasisi. Amebainisha kuwa viongozi wa menejimenti wanapaswa kutambua vipaji vilivyopo, kuvilea na kuvijengea uwezo mapema ili kuendeleza ufanisi wa utendaji, uwajibikaji na uendelevu wa chuo kwa muda mrefu. Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Dkt. Mike Salu alifafanua kwa kina malengo na hatua za uendelezaji wa mpango wa uongozi wa kurithisha madaraka, huku akisisitiza umuhimu wa kuwa na mifumo ya wazi, mipango ya maandalizi ya viongozi mbadala, na tathmini endelevu ya uwezo wa viongozi ili kuhakikisha taasisi inaendelea kuwa imara. Mafunzo hayo yameongeza uelewa wa wajumbe wa menejimenti kuhusu umuhimu wa mipango ya uendelezaji wa uongozi kama chachu ya kuimarisha utawala bora, uwajibikaji na maendeleo endelevu ya Chuo Kikuu Mzumbe.