News-Details

News >Details

WANAFUNZI WA MWAKA WA KWANZA MZUMBE WAASWA KUJENGA MUSTAKABALI WAO KWA MAADILI, BIDII NA UBUNIFU

WANAFUNZI WA MWAKA WA KWANZA MZUMBE WAASWA KUJENGA MUSTAKABALI WAO KWA MAADILI, BIDII NA UBUNIFU

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. William Mwegoha, amewataka wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa mwaka wa masomo 2025/2026 kutumia elimu ya chuo kikuu kama nyenzo ya kujijenga binafsi na kuchangia maendeleo ya jamii, akisisitiza umuhimu wa kuzingatia maadili, nidhamu, uwajibikaji na matumizi sahihi ya uhuru wanaoupata baada ya kujiunga na elimu ya juu. Akizungumza katika kikao kilichofanyika leo tarehe 28 Januari 2026, katika Kampasi Kuu ya Morogoro, Prof. Mwegoha alisema maisha ya chuo kikuu yanahitaji mwanafunzi kuwa na nidhamu binafsi, uwajibikaji na uelewa mpana wa wajibu wake, akibainisha kuwa mafanikio ya kitaaluma hayawezi kupatikana bila misingi imara ya maadili na mwenendo unaokubalika katika jamii. Aidha, Prof. Mwegoha alieleza kuwa falsafa ya mafunzo ya Chuo Kikuu Mzumbe inalenga kumwandaa mwanafunzi kwa vitendo, kwa kuhimiza ujifunzaji unaojengwa juu ya kufikiri kwa kina, kuuliza maswali, kufanya kazi kwa pamoja na kutumia teknolojia kama nyenzo ya ubunifu na ubora wa kitaaluma. “Tunataka muwe wanafunzi wenye maadili, wabunifu na watatuzi wa changamoto za jamii. Elimu mnayoipata hapa isiishie kwenye vyeti pekee, bali iwe na tija kwa jamii mnayotoka,” alisema Profesa Mwegoha. Kuhusu maendeleo ya chuo, Profesa Mwegoha alisema Chuo Kikuu Mzumbe kinaendelea kupanuka kwa miundombinu na programu za masomo, kikiwa na kampasi katika mikoa ya Morogoro, Mbeya na Dar es Salaam, huku maandalizi ya Kampasi ya Tanga yakiendelea ili kuanza kupokea wanafunzi katika mwaka ujao wa masomo. Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe – Taaluma, Utafiti na Ushauri, Profesa Hawa Tundui, aliwakumbusha wanafunzi wa mwaka wa kwanza kuwa kujiunga na chuo kikuu kunahitaji mabadiliko ya fikra, nidhamu ya juu na uwajibikaji binafsi. Alisisitiza kuwa mwanafunzi anapaswa kujitambua mapema kuhusu lengo lake la kitaaluma na mustakabali anaouandaa baada ya kuhitimu. Vilevile, aliwahimiza wanafunzi kutumia teknolojia na Akili Mnemba kama nyenzo ya kuongeza uelewa katika kujifunza na si mbadala wa uwezo wao wa kufikiri, akisisitiza kuwa matumizi yasiyo sahihi ya teknolojia yanaweza kudhoofisha uadilifu wa kitaaluma. Aliongeza kuwa pamoja na ufaulu wa kitaaluma, wanafunzi wanapaswa kujijengea ujuzi laini (soft skills) ikiwemo kujiamini, mawasiliano, kazi kwa timu na uwezo wa kujieleza, akibainisha kuwa ujuzi huo ndio msingi wa ushindani katika soko la ajira na mazingira ya kazi ya sasa. Naye, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe – Mipango, Fedha na Utawala, Prof. Allen Mushi, aliwaeleza wanafunzi kuwa chuo kinaendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuishi ili kuhakikisha kunakuwepo na mazingira rafiki, salama na yenye hadhi ya elimu ya juu. Alisema chuo kimefanya ukarabati na maboresho makubwa ya miundombinu ikiwemo hosteli, kumbi za mihadhara, kafeteria na maeneo ya huduma, huku akibainisha kuwa mazingira ya Mzumbe yaliyopo Wilaya ya Mvomero ni tulivu na yanafaa kwa masomo makini na maendeleo ya kitaaluma. Aidha, alisisitiza kuwa chuo kinaendesha utamaduni wa open door policy, hivyo changamoto zozote zinapaswa kuwasilishwa kwa viongozi husika ili zipatiwe ufumbuzi kwa njia rasmi, badala ya kuzisambaza kupitia mitandao ya kijamii. Pia, Rais wa Serikali ya Wanafunzi Chuo Kikuu Mzumbe Bw. Samwel Chacha aliwataka wanafunzi kuendelea kudumisha amani, umoja na nidhamu chuoni kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za chuo, akisisitiza kuwa kila mwanafunzi ana wajibu wa kuwa balozi mwema wa Chuo Kikuu Mzumbe kwa vitendo na kauli, kwa kuishi kulingana na kauli mbiu ya chuo “Tujifunze kwa Maendeleo ya Watu.” Kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza, safari ya chuo ni fursa ya kujenga mustakabali imara. Nidhamu, maadili mema, ubunifu na bidii ni misingi ya mafanikio. Kila mwanafunzi anaagizwa kuwa balozi wa Chuo Kikuu Mzumbe, akitumia elimu yake kuleta mabadiliko chanya kwa jamii na Taifa.

None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None